July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mambo 6 yamponza Miss Tanzania 2020

Miss Tanzania 2020, Rose Manfere

Spread the love

 

KAMATI ya Miss Tanzania imebainisha makosa sita yaliyosababisha Miss Tanzania 2020, Rose Manfere kuvuliwa uwakilishi wa nchi katika mashindano ya urembo duniani. Anaripoti Matilda Peter, Dar es Salaam … (endelea).

Makosa hayo ni; kuunda menejimenti yake nje ya mkataba, kukiuka maelekezo ya kampuni ya The Look ambao pia ni wasimamizi wa mashindano hayo na kufanya matangazo ya biashara, kupingana na taratibu anazopewa za jinsi ya kushirikiana na wadhamini wa shindano ili kulinda maslahi yake na ya kampuni.

Pia, amekuwa akisuasua kuhudhuria kwenye matamasha ambayo anaalikwa mengine hufika na mengine kufika kwa kuchelewa kitu ambacho kimejirudia zaidi ya mara moja.

Hayo yamebainishwa leo Jumamosi, tarehe 17 Julai 2021 na Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Azama Mwasango, wakati akizungumza sababu za kumweka kando Rose, kwenda kuiwakilisha nchi duniani.

Baada ya kuweka kando, Miss Tanzania 2020, namba mbili, Juliana Rugamisa ndiye ameteuliwa kwenda kuwakilisha nchi hiyo kwenye mashindano hayo ya dunia.

Mwasango amesema, “kuna matangazo ambayo amewahi kuyafanya ambayo ni kinyume na kanuni zetu sisi kama The Look, kwasababu yeye anabeba taswira ya kampuni.”

“Chochote ambacho anakifanya ni lazima kipitie katika kamati yetu tutoe ruhusa ili yeye aweze kuendelea na hayo matangazo,” amesema Mwasango.

“Lakini pia, ameunda menejmenti yake binafsi, bila kuhusiha uongozi wa kamati ya Miss Tanzania ambapo amekuwa akiitambulisha kama kampuni ya The Look inayosimamia uwakilishi wake.”

Mwenyekiti huyo amesema, jambo hilo ni kosa la jinai kwani ameitambulisha sehemu mbalimbali ikiwemo wizara ya habari.

Amesema, Rose ataendelea kuwa Miss Tanzania 2020, lakini kwenye atakosa fursa hiyo ya kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya dunia kutokana na sababu hizo zilizobainishwa.

Uamuzi wa kumwengua Rose, yalitangazwa tarehe 14 Julai 2021, kupitia ukurasa wa Twitter wa Miss Tanzania na kueleza

Jana Ijumaa, tarehe 16 Julai 2021, Rose alifika ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), jijini Dar es Salaam, baada ya kuitikia wito wa kufika ofisini hapo.

Mara baada ya kumaliza mazungumzo, Rose alisema anaiachia Basata kutoa taarifa rasmi ya nini kinaendelea.

Hata hivyo, tayari kamati ya Miss Tanzania, kwa maelekezo ya Basata imekwisha kupeleka jina la Juliana na maandalizi ya kumuandaa kwenda kwenye mashindano hayo yamekwisha kuanza.

error: Content is protected !!