Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari Mambo 6 yajayo Bunge la Bajeti
HabariTangulizi

Mambo 6 yajayo Bunge la Bajeti

Bunge la Tanzania
Spread the love

 

SAFARI ya siku zaidi ya 90 ya mkutano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaanza kesho Jumanne saa 3:00 asubuhi, tarehe 30 Machi 2021, jijini Dodoma. Anaripoti Regina Mkonde, Dodoma…(endelea).

Ni mkutano mahususi kwa ajili wa kujadili mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2020/21, inakadiriwa kufikia Sh. 36.3 trilioni.

Mkutano huo, unaanza kipindi ambacho bado Taifa, linaomboleza kifo cha Dk. John Magufuli kilichotokea Jumatano ya tarehe 17 Machi 2021.

Mwili wa Dk. Magufuli (61), aliyeongoza Tanzania kwa miaka mitano na miezi mitano, kuanzia tarehe 5 Novemba 2021 hadi mauti, ulizikwa nyumbani kwao, Chato mkoani Geita, Ijumaa iliyopita ya 26 Machi 2021.

Bado taifa hilo la ukanda wa Afrika Mashariki, linaomboleza siku 21 za kifo hicho, zitakazohitimishwa 7 Aprili 2021.

MwanaHALISI Online, linagusia baadhi ya mambo ambayo yanatarajiwa kujitokeza katika kipindi cha mkutano huo wa Bunge la Bajeti.

Bajeti 2020/21

Katika mwaka wa fedha 2020/21, Serikali imepanga kukusanya na kutumia kiasi cha Sh.36.3 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asimilia nne, ikilinganishwa na Sh. 34.9 trilioni ya mwaka 2020/21.

Tarehe 11 Machi 2021, Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania, Dk. Phillip Mpango, aliwasilisha mapendekezo ya serikali ya mpango, kiwango na ukomo wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, kwa wabunge jijini Dodoma.

“Kwa kuzingatia sera, misingi na vigezo vya ukomo, jumla ya Sh.36.3 trilioni, zinatarajiwa kukusanywa kwa mwaka 2021/22, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 4.0 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2020/21,” alisema Dk. Mpango.

Waziri wa Fedha, Dr Philip Mpango

Katika mwaka 2020/2021, serikali ilipanga kukusanya na kutumia Sh. 34.9 trilioni, ikijumuisha mapato ya ndani ya Sh. 24.1 trilioni na mikopo nafuu Sh.2.9 trilioni, mikopo ya ndani Sh. 4.9 trilioni na mikopo yenye masharti ya kibiashara Sh.3.0 trilioni.

Dk. Mpango amesema, katika mwaka huo wa fedha unatarajiwa kufika tamati Juni 2021, Serikali ilipanga kutumia Sh.22.1 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh.12.8 trilioni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Kwa maana hiyo, wabunge watakuwa na kazi ya kujadili bajeti hiyo kuu, itakayowasilishwa mwishoni mwa Juni na kwa kuanzia kesho na itakuwa ni mjadala wa bajeti za wizara mbalimbali.

Kifo cha Dk. Magufuli

Kwa mara ya kwanza, Tanzania imempoteza rais aliyekuwa madarakani, Dk. John Magufuli kwa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo wake.

Alifikwa na mauti saa 12:00 jioni ya Jumatano, tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam na kuzikwa nyumbani kwao, Chato mkoani Geita, Ijumaa ya tarehe 26 Machi 2021.

Dk. Magufuli alilizindua Bunge hilo la 12, linaloongozwa na Spika Job Ndugai tarehe 13 Novemba 2020.

Mwili wa Dk. Magufuli, ulipelekwa viwanja vya Bunge jijini Dodoma, tarehe 22 Machi 2021, ili kutoa fursa kwa wabunge na watumishi wa Bunge kutoa heshima zao za mwisho.

Spika Ndugai, akizungumza siku hiyo alisema, wametenga kesho Jumanne tarehe 30 Machi 2021, kuwa siku maalumu ya kuweka azimio la kumuenzi kiongozi huyo.

“Tumetenga tarehe 30 siku tutakayoanza Bunge hapa, tutakuwa na programu maalumu ambayo tutaifanya ndani ya ukumbi wa Bunge ambapo kutakuwa na azimio maalumu,” alisema Spika Ndugai.

Hotuba ya Rais

Mara baada ya kifo cha Dk. Magufuli, aliyekuwa makamu wake wa urais, Samia Suluhu Hassan, aliapishwa tarehe 19 Machi 2021, Ikulu ya Dar es Salaam, kuwa Rais wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba.

Ingawa bado haijawekwa wazi kama Rais Samia, atakwenda kuhutubia mkutano huu wa Bunge utakaodumu kwa miezi mitatu, lakini Spika Ndugai amkaribisha Rais Samia bungeni.

Spika Ndugai tayari amemkaribisha bungeni huku akimhakikishia ushirikiano wa kutosha.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Saluhu akihutubia Taifa mara baada ya kuapishwa

Spika Ndugai alitoa ukaribisho huo Ijumaa ya tarehe 26 Machi 2021, siku ambayo mwili wa Dk. Magufuli, ulikuwa ukizikwa nyumbani kwao, Chato, wakati, kiongozi huyo wa Bunge, akitoa salamu za Bunge.

”Tunamkaribisha bungeni, pale ndipo ataweza kuongea na Watanzania wote. Tunakukaribisha kwa muda utakaoona wewe unafaa,” alisema Spika Ndugai

Makamu wa Rais

Pamoja na shughuli zingine, mkutano huu huu wa Bunge, unatarajiwa kuidhinisha jina la makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo litakuwa limewasilishwa bungeni na Rais Samia Suluhu Hassan.

Ibara ya 37 (5) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza, kiti cha rais kikiwa wazi kutokana na sababu yoyote ikiwemo maradhi au kifo, makamu ataapishwa, kuwa Rais, kwa muda uliobaki.

Dk. Magufuli hadi anafikwa na mauti, alikuwa ameongoza miezi takribani minne na nusu hivyo, rais ataongoza Tanzania kwa miaka minne na nusu iliyobaki hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Sehemu ya Ibara hiyo inaeleza “…kisha baada ya kushauriana na chama cha siasa anachotoka, Rais atapendekeza jina la mtu atakayekuwa makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia 50 ya wabunge wote.”

Hii ina maana, mkutano huo utakaoanza kesho hadi mwishoni mwa Juni 2021, litakuwa na jukumu la kuthibitisha jina hilo la makamu wa Rais.

Baraza la Mawaziri

Jambo lingine ambalo linaweza kujitokeza katika mkutano huu ni mabadiliko ya baraza la mawaziri.

Kumekuwapo na mjadala kwamba, baada ya kifo cha Rais Magufuli, basi baraza lililopo la mawaziri, linapaswa kujiuzulu hususan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Miongoni mwa wanaozungumizia hoja hiyo ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema, Majaliwa anapaswa kujizulu ili kutoa nafasi kwa Rais Samia kuunda baraza lake jipya la mawaziri.

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania

Mbatia amesema, baraza lililopo akiwemo Majaliwa, waliapa mbele ya Dk. Magufuli “na kwa maana hiyo, waziri mkuu, anapaswa kujizulu ili Rais samia, naye aunde baraza lake sasa.”

Hoja kama hiyo, imetolewa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kikisema, baraza lililopo sasa halina uhalali wa kisheria kwani kiapo walichoapa mbele ya Dk. Magufuli “hakiwezi kuhamishwa kwenda kwa Rais mwingine.”

Ikiwa hoja hiyo ikifanyiwa kazi, Rais Samia kuteua waziri mkuu mwingine iwe kuendelea na Majaliwa au la, basi mkutano huu wa Bunge, utakuwa na kazi ya kuthibitisha jina la waziri mkuu, litakalokuwa limewasilishwa bungeni.

Ripoti ya CAG

Pia, mkutano huu wa Bunge, utapokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Ripoti hiyo, tayari imewasilishwa jana Jumapili tarehe 28 Machi 2021, kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere akikabidhi eitabu cha repot kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

CAG Charles Kichere, ndiye aliyewasilisha ripoti hiyo kwa Rais Samia na ndiye ataiwasilisha bungeni wiki ya pili baada ya mkutano wa bungeni wa bajeti kuanza.

Mara baada ya ripoti hizo kuwasilishwa bungeni, zinakabidhiwa kwa kamati za kisekta hususan Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kwa ajili ya kuzichambua.

Kuwasilishwa bungeni kwa ripoti hizo, kunaifanya kuwa mali ya umma hivyo, kutoa fursa kwa vyombo vya habari na makundi mbalimbali kuzichambua watakavyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the love  TUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!