May 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mama Samia: Akisimama Mkapa, shughuli imeisha

Spread the love

MAMA Samia Suluhu Hassam, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameeleza kufadhaishwa na kifo cha Benjamin Mkapa, Rais wa awamu ya tatu. Anaripoti Yusuph Katimba, Dar es Salaam … (endelea).

Kauli hiyo ameitoa leo Jumamosi tarehe 25 Julai 2020, alipofika nyumbani kwa Mkapa, Masaki jijini Dar es Salaam kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Mkapa amefariki dunia usiku wa kuamkia jana Ijumaa tarehe 24 Julai 2020 na mwili wake, utazikwa Jumatano tarehe 29 Julai 2020, kijijini kwake Lupaso Mkoa wa Mtwara.

“Kama kuna jambo kubwa la nchi, akisimama Mkapa basi tunajua suluhi itapatikana. Afrika imepata mshutuo. Kwa hiyo ni kazi ya Mungu, hatuna budi kuipokea.”

“Tumepoteza mtu muhimu na sasa kinachofuata baada ya kifo chake ni kufuata fikra zake, mienendo na miongozo yake katika kuiongoza nchi hii,” amesema Mama Samia.

Amesema, kifo cha Mzee Mkapa kinashtua kwa kuwa, taarifa za kuumwa kwake hazikujulikana na kwamba msiba huo umekuja ghafla.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akisaini kitabu cha maombolezo

“Hatukusikia kuumwa kwake, msiba mzito umekuja kwa ghafla. Huu ni msiba mzito kwa nchi yetu na umekuja kwa ghafla. Tunapaswa kumuombea Mungu ampokee kwa salama,” amesema Mama Samia.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online na MwanaHALISI TV kwa habari mbalimbali

error: Content is protected !!