MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassani, amewataka wanawake nchini humo, kujitosa kwenye nafasi za uongozi kwenye sekta binafsi, ili kuleta usawa wa kijinsia katika utoaji uamuzi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Mama Samia ametoa wito huo leo Jumatatu tarehe 8 Machi 2021, katika Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani, yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, mkoani Dar es Salaam.
“Bado tuna kazi kubwa ya kuingia katika nafasi za maamuzi kwenye maeneo mengine hasa private sector (sekta binafsi), sekta binafsi tunasema ndio injini ya uchumi wa Tanzania. Ili kujenga uchumi, lazima tuwepo juu kufanya maamuzi,” amehimiza Mama Samia.
Ametoa wito kwa jamii, kuwajengea uwezo watoto wa kike, ili wapate uzoefu wa uongozi.
“Lazima tuhangaike, tujipinde watoto wetu waweze kuingia huko, lazima tuingie sababu tukichangia wanawake na wanaume kufanya maamuzi, ndiyo usawa unapatikana.
“Tukiacha jinsia moja kujipendelea kupo, tumewaachia kwa muda mrefu wajipendelee. Sasa tubane bane kidogo mabadiliko yajitokeze,” amesema Mama Samia.
Hata hivyo, amesema serikali imefanikiwa kuweka usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi za kisiasa.
Amesema, Rais wa Tanzania, John Magufuli ni mwanaume huku makamu wa rais akiwa mwanamke, na Spika wa Bunge ni mwanaume (Job Ndugai), wakati naibu wake akiwa mwanamke (Dk. Tulia Ackson).
“Wanawake katika nafasi za maamuzi tumefanya vizuri sana kisiasa, kwenye nyanja za kisiasa leo tunasimama kusema serikali imefanya vizuri sana.”
“Tuna rais mwanamume makamu wa rais mwanamke, spika mwanaume naibu mwanamke,” amesema Mama Samia.
Leave a comment