July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Malipo vipimo Covid-19 Tanzania, iwe huduma na siyo fursa

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam 'Terminal 3'

Spread the love

 

NI takribani mwaka na nusu sasa, dunia inateseka kutokana na ugonjwa wa Covid-19, ambao historia inaonesha ulianzia katika mji wa Wuhan nchini China na kusababisha vifo vingi. Anaandika Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na tasisi nyingine za masuala ya afya, zimeweka bayana kuwa hadi sasa hakuna tiba ya Covid-19 hali ambayo inaweka dunia katika mazingira magumu.

Taarifa za WHO zinabainisha, watu milioni 3.9 wameshafariki dunia huku maambukizi yakiwapata zaidi ya watu milioni 184.6 duniani kote.

Katika nchi ya India hadi sasa zaidi ya watu milioni 30.4 wamepata maambukizi huku zaidi ya watu 398,000 wamefariki dunia na milioni 9.4 wamepona.

Hali ya maambukizi imetapakaa kila pande ya dunia na kusababisha shughuli nyingi za uzalishaji kudorora na kusababisha uchumi kushuka. Kwa sasa limekuja wimbi la tatu la ugonjwa huo.

Kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati hali ya maambukizi imeendelea kuongezeka, ambapo baadhi ya nchi zimeonesha dhamira katika mapambano kwa kuhakikisha wananchi wake wanajilinda kwa kuvaa barakoa, kuepuka mikusanyiko na kuwepo muda wa kuzunguka mitaani.

Katika mapambano ya Covid-19, nchi zote duniani zinatumia mifumo ya kupima wananchi wake hasa wale wanaotaka kusafiri ili kuhakikisha maambukizi hayasambai zaidi.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Aidha, zipo nchi ambazo kwa sasa zinatumia chanjo ikiwa ni mikakati ya kukabiliana na maambuzki hayo ndani ya nchi husika.

Katika hili la kupima Covid-19 kuna changamoto hususan nchini Tanzania ambapo kiuhalisia haioneshi kutilia maanani kupambana na maambukizi, lakini itanataka kujua walioambukizwa au wasioambukizwa kupitia safari.

Kwenye mchakato wa kupima, mwananchi anayetaka kusafiri nje ya Tanzania, unahitajika kuwa na dola 100 sawa na Sh. 230,000 ya Tanzania kiasi cha fedha ambacho kinalalamikiwa kuwa ni kikubwa hasa ikizingatiwa hii ni huduma sio biashara.

Baada ya kupima majibu yakitoka yakionesha huna maambukizi unaweza kusafiri kwenda nje ambapo huko kwa baadhi ya nchi zinatumia majibu yaliyotolewa na mamlaka za Tanzania kukuruhusu uingie bila kupima.

Kwa mfano, Kenya wanatumia majibu ambayo msafiri amepewa Tanzania kukuruhusu kuingia nchini humo, lakini Tanzania haitaki majibu ambayo mtu amepimwa Kenya kuingia nchini humo.

Mwanzoni nililisikia tu watu wakilalamika, lakini binafsi nimelishuhudia mwenyewe ambapo nilifanikiwa kusafiri hivi karibuni kwa kutumia majibu ya vipimo vya Wizara ya Afya, Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nikaruhusiwa kuingia Kenya.

Niliporejea nyumbani, lakini jambo la kushangaza ni kwamba majibu ya vipimo nilivyopatiwa Kenya, nilipofika Tanzania yalikatiliwa.

Nilipofika Tanzania, nikaambiwa nipime tena kwa kutoa dola 25 sawa na Sh. 57,700 au 58,000 jambo ambalo lilinisikitisha na kunikasirisha.

Hali hiyo ilinishangaza kwa sababu Kenya wapo tayari kuwapokea abiria wanaoingia nchini humo wakitokea Tanzania ambao wamepima siku mbili kabla, lakini Tanzania haipo tayari kupokea watu kutoka Kenya au Wakenya waliopima saa 10 zilizopita, hii sio sawa ni uonevu na unyonyaji.

Ni uonevu ambao hauvumiliki kwani haingii akilini nchi ambayo ipo makini na mapambano dhidi ya virusi vya ugonjwa huo inakubali majibu ya nchi ambayo haipo makini zaidi, lazima tujitathmini.

Serikali ya Kenya inapambana na maambukizi ya Covid-19 kwa asilimia kubwa kwani saa 24 wananchi wake wamevaa barakoa, wanaepuka mikusanyiko isiyo na sababu, saa nne usiku wote wapo ndani jambo ambalo kwetu ni kinyume.

Inawezekana nchi yetu imepata chanzo cha kukusanya mapato mengi kupitia Covid-19, lakini kusema ukweli wasafiri wanaonewa kwa kurundikiwa gharama kubwa zisizo na sababu za msingi. Msafiri analazimika kutumia takribani Sh.300,000 kwa safari moja hii sio sawa.

Dk. Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hata kama mna miradi ya kutekeleza lakini siyo kwa kuwakamua wasafiri kiasi hiki. Si kila anayekwenda nje anakwenda kunufaika kwamba anafedha za kutoa tu.

Ingependeza nguvu hiyo mnayotumia kukusanya mapato kupitia Covid-19, iwekezwe kwenye mapambano kwa kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa kufuata njia sahihi za kujikinga na ugonjwa huo.

Wakati nalipishwa mara mbili kipimo na nikiwa nimevaa barakoa nje ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA), wamejaa watu ambao hawachukui tahadhari huu ni utani ambao tunapaswa kuuondoa kwanza ndio tufikirie mapato ambayo yanaonekana ndio kipaumbele.

Nakumbuka siku nimerudi nimepimwa Covid-19 kwa njia ya haraka (Express) ila ndani ya dalala najikuta mimi ambaye nimeambiwa niko salama ndiye peke yangu nimevaa barakoa.

Nimalize kwa kusema Tanzania isitumie COVID-U19 kama kitega uchumi bali ijikite kwenye kuzuia maambukizi, kwani hakuna shaka kuwa tahadhari za kupambana na gonjwa hili zinachukuliwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wachache huku asilimia 95 ya Watanzania wakiishi watakavyo.

Kwa kuwa Serikali imekiri kuwa Covid -19 ipo sioni sababu ya kuendelea kufikiria kukusanya mapato na sio kukabiliana na tatizo, wenzetu majirani wanapambana na maambukizi ndio maana hata gharama zao za kupima ni nusu ya kwetu.

error: Content is protected !!