SERIKALI imekiagiza Chama Kikuu Cha Ushirika (Nyanza) mkoani Mwanza kuhakikisha kinaorodhesha na kuzitambua mali zote za chama hicho zilizokuwa zimetaifishwa kinyemera. Anaripoti Moses Mseti, Mwanza … (endelea).
Imesema mali zote za Nyanza ambazo tayari zimerejeshwa kwenye chama hicho, pia zinapaswa kukatiwa hati miliki hatua ambayo itasaidia kuzitambua na kuondoa mianya ya upigaji.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella, wakati wa mkutano mkuu wa 27 wa chama cha kikuu cha ushirika Nyanza uliofanyika jijini Mwanza.
Mkuu huyo wa mkoa ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole, alisema mali zote zilizopo zinapaswa kulindwa na kuboreshwa na kutangazwa ili zipate wawekezaji.
“Mali zilizopo zinatakiwa kuboreshwa na zitangazwe kwa ajili ya kupata wawekezaji kwa ajili ya kusaidia uendelezwaji wake kwa manufaa ya chama na umma kwa ujumla.
“Mali ambazo pia hazina bima zikatiwe bima mapema iwezekanavyo na zile hujuma zote ambazo zilikuwa zinafanywa na viongozi ziachwe mara moja,” alisema Kipole.
Meneja mkuu wa Chama Kikuu Cha Ushirika Nyanza, Juma Mokili, alisema kuwa thamani za mali zote za chama hicho zilizorejeshwa ni zaidi ya Sh. 15. 853 bilioni.
Alisema kuwa baada ya Rais John Magufuli kuagiza mali za Nyanza kurejeshwa mwaka 2017, tayari walianza kazi hiyo kwa ushirikiano wa ofisi ya Mkuu wa mkoa pamoja na wizara ya kilimo.
Mokili alisema tayari urejeshwaji wa mali hizo umefanyika kwa asilimia 99 na kwamba Machi mwaka huu mali zote ambazo hawajapewa hati zake watakuwa wamekabidhiwa.
Alizitaja baadhi ya mali ambazo zimerejeshwa kuwa ni pamoja na kiwanda cha New Era, jengo la Kauma kilipo kituo cha mafuta cha City Filling Station na kiwanda cha mkonge na Dengu Igogo Mwanza.
“Mali nyingine zilizorejeshwa ni maghara ya mazao kilichopo katika kiwanja namba 104, nyumba tatu zilizopo Isamilo katika viwanja namba 89, 80 na 110,” alisema Mokili.
Mkutano huo uliokuwa na kauli mbiu “ushirika ni afya na uzingatiaji kanuni 10 za kilimo bora cha pamba utawezesha uzalishaji wenye tija,” umewakuta wadau wa kilimo na viongozi mbalimbali.
Leave a comment