July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maleria bado tishio Afrika

Mbu wanaoeneza maleria

Spread the love

Leo tarehe 25 Aprili 2015 Tanzania inaungana na mataifa mengine  dunia kuazimisha Siku ya Malaria Duniani. Siku hii imeanzishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kutoa nafasi kwa wadau kutoa elimu na uelewa kuhusu ugonjwa wa Malaria, ikiwa ni pamoja na kushirikisha jamii, taasisi na wadau mbalimbali juu ya mikakati ya jinsi ya kudhibiti ugonjwa huu, kuonyesha uzoefu, kuangalia changamoto na kupima  mafanikio ya utekelezaji wa mikakati hiyo ya kupunguza na kuteketeza ugonjwa huu.

Kutokana na juhudi za miaka ya nyuma, kiwango cha vifo vya watoto barani Afrika vimepungua kwa 58% tangu mwaka 2000. Hii ni habari njema hata hivyo wadau hawapaswi kusinzia bali kuongeza nguvu kupambana na Malaria.

Kauli mbiu ya mwaka huu 2015 ni “Invest in the future, defeat malaria” ikimaanisha “wekeza kwa maisha ya baadae, tokomeza Malaria”. Kauli mbiu hii imetokana na mafanikio ya huko nyuma. Utafiti umeonyesha kuwa nguvu zaidi zikiongezwa katika upambanaji na malaria kutakuwa a mafanikio mazuri zaidi.

Uzidishaji juhudi katika mapambano dhidi ya Malaria yana umuhimu wa pekee, ukizingatia moja ya malengo ya Milinia (MDGs) ni pamoja na kuondoa Malaria kwa nchi 35 zaidi, ifikapo mwaka 2030.

Madhara ya Malaria

Malaria inamadhara makubwa ya kiuchumi kwenye jamii zetu ambazo tayari zinamatatizo mengi.

Pamoja na juhudi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na njia za kisasa za kujikinga, njia za kisasa za kugundua ugonjwa huu na matibabu mbalimbali, bado kuna matatizo makubwa yanayotokana na ugonjwa huu.

Mataifa ya nchi nyingi hasa za Afrika yanamzigo mkubwa wa kukabiliana na ugonjwa huu. Kwa Afrika peke yake ambapo takribani asilimia  80 ya wagonjwa wote duniani wanatoka, malaria inasababisha ‘hasara ya uzalishaji’ inayofikia dola za Marekani bilioni 12 kila mwaka huku baadhi ya nchi za Afrika zikitumia mpaka 40% ya bajeti ya wizara ya Afya kwa mwaka katika matibabu ya wagonjwa wa malaria.

Malaria inapoteza maisha, inawafanya wafanyakazi, wanafunzi nk. washindwe kuhudhuria kazini na mashuleni na hivyo kupunguza uzalishaji, na kushindwa kuandaa viongozi na jamii ya kesho. 

WHO inakisia kuwa mwaka 2013 kulikuwa na watu milioni 198 walioambukizwa malaria na kati yao watu 584,000 walipoteza maisha, huku mtoto mmoja anafariki kila dakika duniani kutokana na malaria.

Kwa mujibu wa jarida la Lancet la Uingereza linaloandika utafiti na habari za afya, limeonyesha wanaoathirika zaidi na malaria ni watoto chini ya miaka 15, na hawa wanafanya asilimia 65 ya waathirika wote.

Chini ya jangwa la Sahara, malaria inaua wajawazito 100,000,huku watoto 200,000 wenye umri chini ya mwaka mmoja  wakipoteza maisha kila mwaka kwa malaria.

Hali inakuwa mbaya zaidi kwa makundi yaliyo kwenye hatari zaidi ya kupata malaria, makundi haya ni watoto, wanawake wajawazito na wagonjwa wenye maambukizi ya HIV.

Malaria kwa wajawazito inasababibisha matatizo mengi hasa kipindi cha miezi mitatu ya kwanza na miezi mitatu ya pili ikiwa ni pamoja na kuharibika kwa mimba, kuzaa mtoto njiti, kupungukiwa na damu n.k.

Mjamzito mwenye maambukizi ya HIV ana nafasi kubwa zaidi ya kumuambukiza mtoto kabla ya kuzaliwa endapo ana malaria, kwani vimelea vya malaria vinashambulia kondo la nyuma na hivyo kurahisisha virusi vya HIV kupenya na kwenda kwa mtoto kirahisi.  Madhara haya hayaishii kwa mtoto tu bali hata mama anakuwa kwenye hatari ya kufa kutokana na maambukizo ya Malaria. SAababu hii ndiyo inayowataka wajawazito kunywa dawa zilizopendekezwa za kuzuia uwezekano wa kupata malaria ili kupunguza madhara haya.

Kwa mujibu wa Amref Health Africa (zamani AMREF), mwaka 2013 kati ya wajawazito milioni 35, ni wajawazito milioni 15 tu walipata dawa za kuwakinga kupata malaria huku waliobaki hawakupata hata dozi moja, hii ni hatari kwani walijifungua bila ya ulinzi wowote wa watoto wao na wao wenyewe.

Hivyo basi kupunguza madhara na hatimaye kutokomeza malaria serikali na wadau wanapaswa kushirikiana kwa kuonyesha utayari wao. Serikali inapaswa kutimiza ahadi zake za kushughulikia tatizo la malaria ili kutimiza haki ya wananchi ya kuwa na afya bora kwa mustakabali wa nchi.

Kuwajibika huku kwa serikali ni pamoja na matumizi mazuri ya fedha zinazotolewa na wafadhiri kwa ajili ya kutokomeza malaria.Tunaitaka serikali isitumie fedha zinazotolewa kwenye kwa manufaa ya wachache.

Katika juhudi hizo Serikali isisahau kushirikisha wananchi katika juhudui hizi kwani hamna serikali yeyote duniani itakayoshinda vita hivi bila ya kushirikisha wananchi, wadau muhimu. Nguvu pia zielekezwe kwa watoto na wanawake wajawazito hasa maeneo yasiyofikika kirahisi huko vijijini, kwa kuwakinga, kugundua malaria kwa haraka na kuwatibu.

Juhudi hizi ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wananchi waliopewa vyandarua wavitumie kikamilifu na wale watakaotumia kwa manufaa mengine waweze kuchukuliwa hatua kwani haya ni mapambano na kwa pamoja tutashinda endapo kuna utayari wa kisiasa.

error: Content is protected !!