
RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango, itafute suluhu ya malalamiko ya wananchi kuhusu viwango vya tozo ya miamala ya simu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Hayo yamesemwa leo Jumatatu, tarehe 19 Julai 2021 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, akitoa ufafanuzi dhidi ya malalamiko hayo, yaliyoibuliwa na makundi mbalimbali ya wananchi.
Ni baada ya tozo hizo kuanza kukatwa tarehe 15 Julai 2021, ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Fedha iliyopitishwa na Bunge la Bajeti kisha kusainiwa na Rais Samia, ili kuanza kutumika.
“Rais ameshaguswa na jambo hili, amesikia maoni ya Watanzania wote na yameshatolewa maelekezo tuyafanyie kazi ambayo wananchi wameyatoa, nitoe raia kwa wananchi kuwa watulivu kwenye jambo hili,” amesema Dk. Mwigulu.
Aidha, Dk. Mwigulu amesema, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameitisha kikao kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa malalamiko hayo.
Soma zaidi:-
“Tuwe watulivu, timu za wataalamu na sisi tutafanyia kazi na kutoa ufafanuzi yanayohitaji elimu. Baada ya kikao kikubwa cha Waziri Majaliwa na viongozi wakuu, kwa kadri ambayo tutaendelea kufanyia kazi jambo hili,” amesema Dk. Mwigulu.
Amesema wataalamu wa wizara hiyo wameelekezwa kuangalia mfumo wa kitaifa wa ulipaji pamoja na sheria ya tozo ya miamala.
Waziri huyo wa fedha amesema, tozo hizo haziwezi kufutwa kama inavyopendekezwa na baadhi ya watu, kwa kuwa sheria yake imepitishwa na Bunge, lakini Serikali itabadilisha kanuni zake ambazo ziko chini ya wizara yake.
“Sababu hii ni sheria ya Bunge, ilishapitishwa na inatakiwa kutekelezwa. Lakini utekelezaji wake unaelekea kwenye kanuni za waziri na zinaangukia upande wangu wa fedha, nitoe rai kwa wananchi kwamba Serikali imesikia maoni yote, tayari tumeendelea kuzifanyia kazi,” amesema Dk. Mwigulu.

Dk. Mwigulu amesema, wizara yake itayafanyia kazi mapendekezo ya wananchi kuhusu tozo hizo.
“Maeneo ambayo wananchi wameweza kutoa ushauri ambayo yanaelezea namna ambayo jambo hili linawagusa, lakini tumepokea maeneo yanayohitaji kufanyiwa uelimishaji ili kuwa na uelewa wa pamoja,”amesema Dk. Mwigulu.
Dk. Mwigulu ameongeza “ikiwa pamoja na viwango vinavyokatwa, yupi na yupi anakatwa. Pamoja na uelewa wa ukataji kunakotumwa na wakati wa kutoa, lakini pia mantiki ya jambo zima kiujumla.”
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile, amesema wizara yake itashirikiana na wizara ya fedha kwa ajili ya kufanyia kazi suala hilo.

Samia Suluhu Hassa
“Na sisi kama wizara, kama sekta imeguswa na tozo na tumekuwa tunakusanya maoni na ushauri. Tumekuwa tunachakata takwimu vilevile tangu tozo ianzishwe niseme wizara itakupa ushirikiano kuhakikisha maelekezo yaliyotolewa na viongozi wetu tutayafanyia kazi,” amesema Dk. Ndugulile.
Tozo hiyo baada ya kuanza kutumika, imekuwa ikipingwa na makundi mbalimbali, ikiwemo vyama vya siasa, asasi za kiraia na wananchi wa kawaida, wakiomba iondolewe au ipunguzwe, ili kuwaondolea mzigo wa makato wananchi hasa wenye kipato cha chini na waishio vijijini.
Kodi na matumizi kwa maendeleo viende sambamba.
Kodi za miamala ya simu zitumike kwenye kimarisha simu vijijini na siyo kuhamishiwa kwingine na kusababisha uizi na uzembe kwenye sekta zingine.
Tuachane na tabia ya sehemu moja itumiwe kubeba sehemu nyingine…huko ni kufilisika kiakili.
Tujenge fikra ya kuwa na ziada (surplus) na siyo kuhamisha, hamisha pesa.
Utalii ulipokuwa na ziada zingeachwa huko huko, leo zingetumika kuuendeleza wakati huu wa Corona.
Kwa maendeleo, kila sekta itoe 20% yake kwa maendeleo! Tuachane na mfumo wa kikoloni!
Tatizo ni nini? Malalamiko ya miamala na tozo ni mengi. Mbona suluhisho lake linachukua muda mrefu hivi kukamilika?