January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makunga mwenyekiti mpya TEF

Spread the love

MHARIRI Mtendaji wa Kampuni ya Jambo Concept, Theophil Makunga amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF). Anaandika Christina Cosmas, Morogoro … (endelea).

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mratibu wa Jukwaa la wahariri (TEF) Prisca Kabendera alisema Makunga ameshinda nafasi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali kwa kupata kura 34 dhidi ya 32 za mpinzani wake, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Nipashe, Jesse Kwayu kati ya kura  66 zilizopigwa.

Kabendera pia alitangaza matokeo ya nafasi ya makamu Mwenyekiti na kumtangaza Deodatus Balile kuwa makamu mwenyekiti baada ya kupata kura 47 dhidi ya mshindani wake Bakari Machumu aliyepata kura 17 kati ya kura 64 zilizopigwa.
Alitangaza nafasi ya Katibu kuchukuliwa na Neville Meena ambaye alikuwa mgombea pekee na katibu msaidizi ilichukuliwa na Nengda Johanes ambaye alikuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo.
Pia Kabendera aliwataja wajumbe waliopita nafasi ya wajumbe wa bodi ni Salim Salim, Jesse Kwayu, Joyce Shebe, Bakari Machum, na Lilian Timbuka.
Wajumbe hao wa bodi ni kati ya wajumbe 9 waliogombea nafasi hiyo wakiwemo Daniel Chongolo, Masiaga Matinyi, Joseph Kulangwa na Eklandi Mwafisi.
Mwenyekiti mstaafu wa Jukwaa hilo Absalom Kibanda ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa uchaguzi huo aliwapongeza wajumbe hao kwa kufanya uchaguzi kwa kuzingatia jenda ambapo wameweza kuwachagua wanawake watatu wote waliogombea nafasi ya ujumbe wa bodi kati ya wanawake tisa waliopo kwenye Jukwaa hilo.
Naye Mgombea mwenza wa nafasi ya Mwenyekiti Jesse Kwayu aliwapongeza wanachama kwa hatua hiyo ya kumchagua mwenzake na kusema kuwa ameyapokea matokeo hayo kwa mikono miwili huku akiahidi kusimamia na kutekeleza aliyoahidi katika TEF.
Aidha Kwayu aliwaasa wanachama hao kuacha marumbano bali wawe kitu kimoja katika kujenga jukwaa hilo na kuleta maendeleo katika tasnia hiyo.
Akizungumzia matokeo hayo Mwenyekiti aliyechaguliwa Makunga alisema aliwashuru wajumbe kwa kumuamini na kumchagua kuwa mwenyekiti na kuahidi kuiinua, kuisimamia na kuiongoza TEF ili iweze kupiga hatua kimaendeleo.
“namshukuru mungu kwamba mmenipa timu ambayo ni nzuri, yenye mtazamo mzuri wa kuongoza vizuri TEF katika kuleta mabadiliko chanya” alisema.
Viongozi hao wote waliochaguliwa wataongoza Jukwaa hilo ndani ya kipindi cha miaka mitatu kwa mujibu wa sheria na kanuni za TEF.

error: Content is protected !!