Saturday , 22 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Makubaliano ya Barrick: Zitto, Serikali nani mkweli?
Habari za SiasaTangulizi

Makubaliano ya Barrick: Zitto, Serikali nani mkweli?

Spread the love

SERIKALI na kampuni ya madini ya Barrick Gold Corporation, wamefikia makubaliano ya kumaliza mgogoro wa kibiashara kwa kuunda kampuni ya pamoja ya madini. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Katika makubaliano hayo, serikali na Barrick, wameafikiana kuunda kampuni ya pamoja ya kufuatilia uchimbaji wa madini katika migodi ya Buzwagi, North Mara na Bulyanhulu.

Kuudwa kwa kampuni hiyo, iliyopewa jina la Twiga Minerals Company Limited (TMCL), kunatajwa na serikali ya Tanzania kuwa kutamaliza mgogoro wa muda mrefu kati yake na kampuni ya Acacia Mining PLC.

Makao makuu ya kampuni ya Twiga Minerals Company Limited, yamepangwa kuwa jijini Mwanza.

Mgogoro kati ya serikali na kampuni ya Acacia, uliibuka mwaka 2017, kufuatia madai kuwa kampuni hiyo ya dhahabu imekuwa ikitorosha nje madini inayozalisha na ukwepaji kodi.

Acacia, ni kampuni tanzu ya Barrick Gold Corporation; katika kumaliza mgogoro kati yake na serikali, tarehe 19 Julai mwaka huu, Barrick ilitangaza kununua hisa zote za Acacia kwa thamani ya Dola za Marekani 428 milioni.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Rais wa kampuni ya Barrick Gold Corporation, Marck Bristow, ameeleza kuwa “makubaliano hayo yamefungua uwanja mpya wa mazingira ya ushirikiano katika uzalishaji wa madini.”

Aidha, Bristow amesema, makubaliano hayo yamemaliza utata wa muda mrefu kati ya serikali ya Tanzania na kampuni ya Acacia.

Amesema, “kuanza upya kwa uzalishaji uliosimama kwa miaka mitatu, kunahitaji uwekezaji mkubwa na rasimali za kutosha. Lakini kwa makubaliano tuliyoyafanya, naamini yatasaidia kusukuma kuanza uzalishaji kwa haraka na kwa kasi.

“Kampuni ya Twiga itasaidia serikali kuwa mwangalizi na mshiriki wa karibu katika kila maamuzi yatakayofanywa kwenye migodi yetu.”

Maridhiano hayo kati ya Barrick na Tanzania, yalifikiwa chini ya mwenyekiti wa kamati ya upatanishi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Prof. Palamagamba Kabudi.

Mgogoro kati ya serikali na Acacia, ulianza mwaka 2017, baada ya Rais John Magufuli, kuunda tume ya kuchunguza mwenendo wa kibiashara wa kampuni hiyo ya madini.

Katika ripoti yake, tume hiyo ya rais ilidai kuwa Barrick na dada yake Acacia, walikuwa wanatenda shughuli zao za kibiashara kinyume cha sheria, jambo ambalo limeikosesha serikali mapato ya Dola za Marekani 190 bilioni.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya uchumi, wameeleza MwanaHALISI ONLINE kuwa makubaliano hayo kati ya serikali na Barrick, ni kama ‘changa la macho.’

Zitto Zuberi Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), amesisitiza kuwa tungeweza kunufaika zaidi, kama Acacia ingenunuliwa wakati ule na kampuni nyingine ya Canada kwa thamani ya Dola za Marekani 4.4 bilioni (Sh. 10 trilioni).

Anasema, “tumeendelea kuibiwa kama ambavyo tumekuwa tukiibiwa huko nyuma. Barrick imeinunua Acacia kwa Dola za Marekani 428 milioni. Kabla ya sakata la makanikia, Machi 2017, Acacia ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani 4,400 Milioni (Sh. 10 trilioni).”

Zitto anasema, “Tungepata kodi ya ongezeko la mtaji la Dola za Marekani 880 milioni (Sh. 2 trilioni). Lakini serikali yetu haikufanya subira na ikazuia makanikia na mpango ule wa Acacia kununuliwa ukavugika.”

Anasema, katika makubaliano hayo, Barrick itailipa serikali ya Tanzania, dola milioni 300 (Sh. 700 bilioni), kama malipo ya kumaliza mgogoro na siyo kishika uchumba kama ilivyoelezwa na serikali bungeni.

Anasema, mkataba uliyofikiwa na pande hizo mbili, Barrick watalipa fedha hizo, kwa muda wa miaka saba na kwamba fedha hizo zitalipwa baada ya kuondoa madai yote ya kodi ambayo Acacia inaidai Tanzania.

Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo anasena, “…Acacia Group ina madai ya marejesho ya kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT Refunds), inayofikia takribani Dola za Marekani 240 milioni (Sh. 552 bilioni.

“Hivyo basi, katika malipo ya dola za Marekani 300 milioni, zitakazobakia baada ya kutoa madai ya VAT ni dola 600 milioni (Sh.138 bilioni tu),” anaeleza.

Anasema, “kibaya zaidi, hata hizi Dola za Marekani 60 milioni hazitatolewa. Hii ni kwa sababu, Barrick Gold wamesamehewa kodi ya ongezeko la mtaji yenye thamani ya dola za Marekani 85.6 milioni. Barrick wamepewa misamaha mbalimbali ya kodi, ikiwamo kodi ya ‘Capital Gains’ ambayo inatokana na mauzo ya hisa za Acacia kwa Barrick.”

Bunge la Jamhuri lilitunga sheria ya kutoa kodi ya ongezeko la mtaji mwaka 2012, kwa mauzo ya mali zilizopo nchini ili kudhibiti ukwepaji wa kodi.

Zitto anasema, “Barrick inainunua Acacia kwa hisa ambazo haikuwa inamiliki na ambazo zimepewa thamani ya dola 428 milioni. Capital Gains Tax ya asilimia 20 ilipaswa kulipwa, lakini msamaha uliotolewa umepoteza mapato hayo halali na ya kisheria ya dola 85.6 milioni (karibu Sh. 200 bilioni).”

Wakati Serikali ya Tanzania ikieleza kunufaika na makubaliano hayo, Zitto anadai kuwa siyo tu kwamba Tanzania kiuhalisia haitapata dola 300 milioni, bali pia tunaipa zawadi Barrick ya dola 25.6 milioni za ziada.

Pia, Zitto amekiri kuwa serikali itapewa hisa za bure ya asilimia 16 kwenye kampuni tanzu zote za Barrick nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Padre anayetuhumiwa mauaji ya Asimwe, asimamishwa

Spread the loveKanisa Katoliki Jimbo la Bukoba limemsimamisha kutoa huduma za kichungaji...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali yaahidi kushirikiana na Prof. Ndakidemi kuhamasisha zao la kahawa

Spread the loveSerikali imeahidi kuungana na Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick...

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

IMF yaimwagia Tanzania trilioni 2.4 kukabili mabadiliko ya hali ya hewa

Spread the loveShirika la Kimataifa la Fedha (IMF) jana Alhamisi limesema bodi...

Habari za SiasaKimataifa

Mmoja afariki, 30 wajeruhiwa maandamano Kenya

Spread the loveMtu mmoja ameripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa...

error: Content is protected !!