SERIKALI imetatua changamoto ya kukwama kwa makontena ya wafanyabiashara wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika Bandari ya Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Akizungumza na wafanyabiashara pamoja na maafisa kutoka ubalozi wa Congo hapa nchini, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe amesema makontena hayo yameanza kutoka bandarini.
Kamwelwe amesema makontena hayo yalizuiliwa kutokana na changamoto iliyojitokeza iliyotokana na utaratibu wa kawaida wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiujiridhisha kuwa mizigo inayotakiwa kutoka nje ya nchi inatoka na haibaki nchini, na kwamba mamlaka hiyo imeshafanyia kazi suala hilo.
Mnamo tarehe 16 Februari 2019 wizara hiyo ilipokea taarifa kuhusu changamoto iliyojitokeza katika uondoshaji wa makasha ya mizigo maarufu kama makontena kutoka bandari ya Dar es Salaam kuelekea Congo.
Baada ya wizara hiyo kupokea changamoto hiyo, Waziri Kamwelwe alimuagiza Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho kuitisha kikao cha dharula kilichohusisha wataalam kutoka wizara yake, TRA na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na wadau wengine ili kujadili changamoto hiyo.
Mwishoni mwa mwaka jana takribani makontena 327 ya wafanyabiashara wa Congo yalizuiwa katika Bandari ya Dar es Salaam, baada ya serikali kubaini kwamba kuna baadhi ya wafanyabaishara wasio waaminifu wanauza bidhaa hizo hapa nchini badala ya kuzipeleka Congo. Miongoni mwa bidhaa hizo ni pamoja na mchele, sukari na mafuta ya kupikia.
Leave a comment