January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makonda, Mbowe wamaliza mgomo wa madereva

Wananchi wakishangilia mara baada ya magari yaendayo mikoani na nchi jirani kuanza safari zake katika kituo Kikuu cha mabasi cha Ubungo. Safari zimeanza baada ya madereva kusitisha mgomo kwa muda hadi kesho saa 4:00 asubuhi ili makubaliano waliyowekeana na serikali yashughurikiwe.

Spread the love

UAMUZI wa kishujaa uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda-kwa upande wa Serikali na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kujadiliana na madereva waliogoma kwa saa 32, umesaidia kusitisha kwa muda mgomo huo na kuwezesha abiria kuendelea na safari. Anaandika Pendo Omary…(endelea).

Hatua hiyo ni baada ya Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kukwepa kukutana na madereva hao kwa kipindi hicho.

Katika kusaka suluhu, Makonda alilazimika kujitwisha zigo hilo kama kiongozi wa Wilaya kilipo kituo kikuu cha mabasi ambapo wagomaji walikusanyika na hivyo kuafikiana kwamba serikali itatekeleza makubaliano hayo kabla ya kesho saa 4:00 asubuhi, vinginevyo wataendelea kugoma.

Baada ya muafaka huo, hatimaye saa 7:00 mchana, mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi yameanza safari zake huku daladala nazo zikianza kubeba abiria katika maeneo mbalimbali katika mikoa yote ambayo kulikuwa na mgomo.

Hatua hiyo, ilifikiwa baada ya kutia saini makubaliano na Umoja wa Madereva Tanzania (TTDA) baada ya majadiliano ya pamoja yaliyodumu takribani saa tatu kati ya viongozi wa madereva, Freeman Mbowe – aliye pia Mwenyekiti wa Chadema na Makonda.

Makubaliano hayo yanahusu “hadi kufikia kesho saa 4: asubuhi kamati iliyoudwa kushughulikia madai ya madereva inapaswa kuwa na; wajumbe wanaofahamika na kuaminika kwa madereva; kuwa na hadidu za rejea na muda maalum wa kamati kufanya kazi”.

Mbowe amesema “Sisi kama vyama vya sisasa tunawajibu na kushiriki kuwezesha katika kudai haki. Tunakubaliana na kitendo cha madereva kugoma. Kwa sababu ndio njia pekee ya kuifanya serikali isikie”.

“Serikali imeahidi mpaka kufikia kesho itatatua tatizo. Tuwape subira, tuwasikilize. Madereva wapeleke abiria katika maeneo mbalimbali ili kurudisha utulivu katika taifa,” amesema Mbowe.

Mbowe alilazimika kuongea baada ya mamia ya madereva na wananchi waliokuwa katika viwanja vya kituo cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi kumtaka kufanya hivyo.

“Tunamtaka Rais Mbowe…tunamtaka Rais Mbowe…Mbowe …Mbowe…,” zilisikika sauti kutoka kwenye umati huo.

Mbowe alilazimika kuzungumza bila kutumia kipaza sauti baada ya kifaa hicho kufichwa na askari polisi ambaye jina lake halikupatikana mara moja kwa madai kwamba Makonda ndiye aliyekikodi na sio Mbowe.

Aidha, Katibu Mkuu wa TTDA, Rashidi Salehe amesema “kupitia makubaliano ya barua hii na Mkuu wa Wilaya, amekubali kuweka sahihi mbele ya viongozi na amesema yupo tayari kuhamasisha mgomo kama makubaliano hayo hayatatekelezwa”.

“Tunaomba viongozi wote walioshiriki kusimamaia haki za hawa madereva asipotee hata mmoja. Zipo njia nyingine tunaweza kulimaliza tatizo, zikatafutwa sababu za kukomoana kwa sababu tumeziona lugha za viongozi zinazotia shaka,” amesema Salehe.

Akizungumza kwa niaba ya serikali, Makonda amesema katika madai yaliyopo imeudwa tume huku uongozi wa TTDA ukishidwa kuitambua tume hiyo wakiwemo wanachama wake. Kwamba hali hiyo imepelekea TTDA kuiwekea tume hiyo masharti.

“Kesho ifikapo saa 4:00 asubuhi, kama hatujui majina ya wajumbe wa kamati, kama hatujui hadidu za rejea zilizopo ndani ya kamati, kama hatujui kamati hiyo itafanya kazi muda gani na kama hatujui wajumbe hao wanatokana na sisi na hatuwaamini. Kesho asubuhi mgomo uendelee,” amesesisitiza Makonda.

Makonda amewataka abiria kutokata tiketi kwa ajili ya safari hapo kesho iwapo muafaka aliokubaliana na TTDA hautafikiwa.

Awali asubuhi, Jeshi la Polisi limelazimika kutumia mabomu ya machozi katika kituo hicho baada ya baadhi ya madereva kuanza kuwarushia mawe viongozi waliofika kwa ajili ya mazungumzo nao, akiwemo Makonda na Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani, DCP Mohamed Mpinga.

Hatua hiyo, imetajwa kuchochewa na madai kuwa ahadi wanazozitoa viongozi wa serikali na wanasiasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) hazina maana, hivyo kutaka Waziri Mkuu afike eneo hilo.

Mgomo huo umeendelea leo asubuhi baada ya Pinda jana kukwama kuwafuata madereva hao Ubungo huku akitaka afuatwe ofsini kwake.

Hata hivyo, baada ya majibu ya Pinda, madereva nao waliwakataza viongozi wao kwenda huko kwa madai “kumekuwepo na mazungumzo mara kwa mara katika ofsi za serikali bila mafanikio huku wakiishia kukamatwa na polisi.”

 “Tarehe 18 Aprili tulipaswa kukutana na serikali. Lakini 17 Aprili, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga, akakutana na wamiliki wa magari ambao ndio watuhumiwa namba moja na kutuacha sisi walalamikaji. Hii ina maana gani,” ameongeza Salehe.

Mbali na kufikiwa kwa makubaliano hayo mgomo huo uliondumu kwa muda wa saa 32 umesababisha kukwama kwa usafirishaji huku wananchi wakilazimika kutumia kati ya Sh. 10,000 hadi Sh. 30,000 kwenda katika shughuli zao kwa siku kwa usafiri wa bajaji au boda boda.

Mbali na kupanda kwa gharama za usafiri pia baadhi ya wanafunzi katika maeneo mbalimbali nchini wameshindwa kufanya mitihani ya kumaliza kidato cha sita.

 

 

error: Content is protected !!