July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makonda kuanzisha mtaa wa bar

Spread the love

PAUL Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, ametangaza mpango mpya wa kuanzisha mtaa maalum utakaokuwa ukihusika na biashara ya uuzaji wa vinywaji vikali na baridi (Bar), anaandika Charles William.

Makonda ameweka wazi mpango huo mapema hii leo jijini Dar es Salaam ikiwa pia ndiyo siku ambayo utekelezwa wa mpango wa walimu wa shule za msingi na sekondari kusafiri bure kupitia usafiri wa umma (daladala) unaanza rasmi.

Mkuu huyo wa wilaya amesema mpango huo ni muendelezo wa ubunifu na uthubutu wa mipango ya maendeleo ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa ukikosekana miongoni mwa Watanzania na hivyo kufanya kasi ya maendeleo hapa nchini kuwa ndogo tofauti na matarajio ya wananchi.

“Kinondoni nina mpango wa kutengeneza mtaa mmoja maalum wenye bar tu ili watu wakitaka kwenda kunywa pombe waende mtaa huo bila kubugudhi. Nasubiri muda tu ufike kwa sababu haiwezekani kila eneo liwe na bar mpaka nyuma ya misikiti na nyuma ya makanisa,” ameeleza Makonda.

Wilaya ya Kinondoni ndiyo wilaya yenye watu wengi zaidi hapa nchini ambapo kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 wilaya hiyo ina jumla ya watu milioni 1.7 na kwasasa ikikadiriwa kufikia watu milioni 1.9.

Katika hatua nyingine pia Makonda ameeleza kuridhishwa na zoezi la walimu wa jiji la Dar es Salaam kuanza kusafiri bure hii leo huku akibainisha changamoto mbalimbali alizozishuhudia hii leo wakati alipotembelea vituo mbalimbali za daladala kuangalia zoezi hilo.

Makonda amesema: “Changamoto zipo ikiwemo baadhi ya walimu kuficha vitambulisho vyao wakati nimewambia wavivae, lakini kiukweli makondakta wote katika vituo vya mawasiliano na Tegeta nilivyotembelea wana hamasa kubwa ya kuwasafirisha walimu kila mahali wanaita, walimu! walimu!”

error: Content is protected !!