January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makonda hana usafi wa kumtuhumu Gwajima

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Spread the love

ANAYEITWA mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, ameelekeza asichokiamini na; anataka kutenda asichokuwa na mamlaka ya kukitekeleza. Anaandika Saed Kubenea … (endelea).

Amesema amemuita ofisi kwake Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ili kueleza maana ya matamshi yake dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Makonda amejigamba kuwa Gwajima anatakiwa “kueleza maana ya uhuru wa kuabudu unaoelezwa katika Katiba (ya Jamhuri ya Muungano), usajili wa taasisi yake na katiba ya taasisi hiyo.”

Amesema, yeye ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni. Ameagiza jeshi la polisi kumkamata Askofu Gwajima ili ahojiwe. Baadaye wamfikishe kwake “ili aeleze maana ya kile alichokieleza.”

Ndani ya ofisi ya Makonda, kiongozi huyo wa kidini anatakiwa kuhojiwa na “jopo la watu 20.”

Ndivyo vyombo vya habari – radio, magazeti, televisheni na mitandao ya kijamii – vilivyomnukuu mkuu wa wilaya ya Kinondoni.

Askofu Gwajima amenukuliwa akimtuhumu Kardinali Pengo kwa madai kuwa amewasaliti wa viongozi wenzake wa Kikristo kwa hatua yake ya kupinga waraka wa maaskofu kuhusu Katiba Pendekezwa na Mahakama ya Kadhi.

Hakuna asiyemfahamu Makonda – mkuu mpya wa wilaya ya Kinondoni. Hakuna! Vitendo vyake; kauli zake na minendo yake, vinafahamika. Hana mamlaka ya kimaadili wala kisheria wa kusimamia anachokieleza.

Rekodi zake zipo na zinajulikana na wengi.

Kwanza, angalau Askofu Gwajima amesema, hatapoteza muda kwenda kumuona Makonda. Barua aliyoipata kutoka katika ofisi yake, hataijibu. Ni barua iliyomfedhehesha; itajibiwa na maombi ya mnyororo yanayoendelea.

Makonda hana mamlaka ya kisheria wala kimaadili ya kumuita Askofu Gwajima.Kama kuna kesi ya jinai, wanaopaswa kuchunguza na kushitaki, ni polisi. Siyo Makonda.

Lakini jambo ambalo liko wazi, ni kuwa ukipitia kauli za Askofu Gwajima dhidi ya Kardinali Pengo, unagundua kuwa alichokitenda ni madai. Siyo jinai; anayepaswa kushitaki au kulalamika katika kaei ya madai, ni Kardinali Pengo. Siyo Makonda, wala Sulemain Kova.

Pili, ni Makonda huyuhuyu, aliyeasisi vurugu, kulipa vijana, kuwaongoza na kisha kushambulia; naye kukiri kumpiga aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba.

Makonda alifanya vurugu hizo katika mdahalo ulioitishwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), tarehe 2 Novemba 2014. Ulifanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam.

Ilikuwa katikati ya mjadala, ambako Jaji Warioba, kwa ustadi mkubwa alianza kupangua hoja moja baada ya nyingine, juu ya maudhui na kilichomo katika Rasimu ya Pili ya Katiba, ambayo ilikuwa imesheheni maoni ya wananchi.

Mbali na vurugu za Makonda kuvunja mdahalo, lakini pia Jaji Warioba – waziri mkuu na makamu wa Rais mstaafu wa Jamhuri – alipigwa na Makonda na wafuasi wake. Karibu wote waliompiga na kumfanyia vurugu Jaji Warioba, ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wakati Makonda anapanga kumshambulia Jaji Warioba, alikuwa anajua kuwa alikuwa anavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inayoruhusu uhuru wa kutoa maoni na kukusanyika.

Aidha, katiba hiyohiyo inatoa uhuru wa Kardinali Pengo kutoa maoni yake kuhusu msimamo wa makanisa; sawa na Gwajima alivyotoa maoni yake kuhusu Kardinali Pengo.

Lakini hata kama Gwajima angekuwa na makosa, Makonda hana mamlaka ya kimaadili wala kisheria ya kusikiliza kesi dhidi ya kiongozi huyo wa kiroho.

Si hivyo tu: Ni Makonda aliyekuwa akiporomosha mvua ya matusi dhidi ya Edward Lowassa na baadhi ya viongozi wa madhehebu ya kidini. Amekuwa akimgombanisha Lowassa na Rais Jakaya Kikwete; Lowassa na chama chake na Lowassa na vyombo vya habari.

Hakuwahi kuhojiwa na jeshi la polisi wala kinachoitwa, “Kamati ya ulinzi na usalama.” Bila shaka alikuwa kazini. Alikuwa anawatumikia waliomtuma.

Hata hivyo, kesi ya Askofu Gwajima, imerejea yaleyale ambayo yamekuwa yakielezwa kwa zaidi ya miaka 15 sasa; hakuna usawa katika taifa. Kumesheheni ukaburu.

Kuna orodha ndefu ya watu wakikashifu mtu mwingine, wanapongezwa kwa kupewa vyeo. Lakini wengine wanatafutwa kwa marungu, kuzuiliwa na kufunguliwa mashitaka.

error: Content is protected !!