August 4, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Makonda aumbuka, azomewa mbele ya JPM

Spread the love

PAUL Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amezomewa na wafanyabiashara wadogowadogo (wamachinga) mbele ya Rais John Magufuli, anaandika Faki Sosi.

Tukio hilo lilitokea jana katika ofisi ndogo za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizopo Mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam baada ya Rais Magufuli kutoka mikoani kwa ziara yake ya kuwashukuru Watanzania.

Wafanyabiashara hao walifika kwenye ofisi hizo wakiwa na mabango yalio na maandishi yenye ujumbe wa malalamiko kwa rais dhidi ya Mgambo wa Jiji wanaowazuia kufanya biashara zao.

Wakati Rais Magufuli akizungumzia suala la mama lishe, wauza mbogamboga na wamachinga kuhusu kusumbuliwa na Mgambo wa Jiji, alisema ameteua viongozi wazuri akiwemo Makonda kama Mkuu wa Mkoa.

Lakini alipotajia jina la Makonda, sauti kutoka kwa wamachinga zilipiga kelele na kusema ‘jipu hilooooo baba,’ kelele hizo ziliendelea.

Rais Magufuli alisita kidogo kuongea kupisha zomea hiyo na baada ya muda mchache aliendelea kuzungumza.

Pamoja na Makonda kuzomewa, Rais Magufuli alisema, hataki kuona makundi hayo yakibaguliwa na kuagiza kuandaliwa kwa utaratibu mwingine.

Wamachinga hao walifika kwenye hadhara hiyo na mabango mbalimbali ambayo moja ya jumbe zilizoonekana kwenye mabango hayo ni pamoja na ‘Kilio chetu kwa Rais JPM ulituahidi ukiingia Ikulu mgambo watafute kazi nyengine…’ na ‘wamachinga tumekosa uhuru’ ambapo Rais Magufuli. Hata hivyo Rais Magufuli aliwataka watulie.

Kadhia ya kuzomewa Makonda mbele ya Rais Magufuli inamfika siku chache baada ya John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuzomewa mbele ya rais huyo.

Mongella alikumbana na kasheshe hiyo wakati akitoa taarifa fupi ya hali ya usalama na shughuli za maendeleo Mkoa wa Mwanza.

Akiendelea kusoma ghafla wananchi hao walianza kumzomea, hatua ya kuzomea ilianza pale Mongella alipodai kwambwa, hakuna njaa katika mkoa huo.

Mongella amedai kuwa, katika mkoa huo wa Mwanza, wamefanikiwa kuvuna chakula kingi na hakuna tatizo la njaa, kitendo ambacho kilipingwa na wananchi hao ambao walisikika wakidai, “acha uongo’ tuna njaa, hakuna chakula.”

error: Content is protected !!