May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makonda atinga makahamani, apewa siku 21

Paul Makonda, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam

Spread the love

 

ALIYEKUWA mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni jijini Dar es Salaam impe muda wa kujibu maombi yaliyofunguliwa na mwanahabari, Saed Kubenea ya kutaka kumfungulia kesi ya jinai. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Maombi hayo yamewasilishwa leo Jumatano, tarehe 2 Machi 2022 mbele ya Hakimu Aron Lyamuya na Goodchance Reginald ambaye ni wakili wa Makonda akisema, amechelewa kupata wito huo kwani ameupata kupitia vyombo vya habari.

“Mteja wangu ameni-engage hivi karibuni kwamba hakupata taarifa yeyote ya summons, ingependeza tungepata summons na muda wa kujibu,” amedai Wakili Reginald.

Ombi hilo lilipingwa na Hekima Mwasipu, Wakili wa Kubenea aliyedai hajaiambia mahakama Makonda taarifa imemfikiaje hadi amemtuma aje kumuwakilisha mahakamani hapo.

Wakili Reginald alijibu pingamizi hilo akidai “mteja wangu alipata hizi habari kupitia vyombo vya habari, akaona si vyema yeye alikuwa kiongozi wa Serikali akaona ni vyema alete wakili lakini summons hajapewa.”

Kutokana na maombi hayo, Hakiumu Lyamuya amempa siku 21 Makonda ili kuwasilisha hati kinzani dhidi ya maombi hayo yaliyofunguliwa na Kubenea.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Subira Mwalumuli, aliieleza mahakama hiyo kuwa wajibu maombi namba moja na mbili, ambao ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), wanatarajia kuleta mapingamizi ya awali dhidi ya maombi hayo.

“Shauri liko kwa ajili ya kutajwa lakini pia tarehe hii ilipangwa kuletwa hati kinzani, kwa wajibu maombi wa kwanza na wa pili wameleta taarifa ya kutoa pingamizi la awali na pingamizi hili la awali ni juu ya shauri lililo mbele ya mahakama yako. Kwa hivyo tunaomba kutoa hiyo taarifa mbele ya mahakama yako,” amedai Wakili Mwalumuli.

Hakimu Lyamuya ameahirisha kesi hiyo hadi tarehe 25 Machi 2022 huku upande wa wajibu maombi namba moja na mbili yaani mkurugenzi wa mashtaka (DPP) na mwanasheria mkuu wa serikali (AG) wakiieleza mahakama hiyo kuwa wanakusudia kuleta pingamizi la awali juu ya maombi hayo.

Katika kesi hiyo, Kubenea anawakilishwa jopo la mawakili wakiongozwa na Nyaronyo Mwita Kicheere na Hekima Mwasipu.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Makonda anadaiwa kuwa siku ya tarehe 17 Machi 2017, akiwa na watu waliobeba silaha za moto, alivamia Clouds TV na kumuagiza mtangazaji wa kipindi cha Shilawadu kurusha video inayomwonesha mwanamke aliyejulikana kwa jina la Grace Athuman.

Katika video hiyo, ambayo haijulikani nani ameiandaa, mwanamke huyo alidaiwa kuonekana akifanya tendo la ndoa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Kwa mujibu wa ushahidi wa video za CCTV, Makonda anaonekana kuvamia kituo cha Clouds saa nne usiku, akiwa anaendesha mwenyewe gari namba T553BFM.

Nyaronyo Kicheere (kulia) na Hekima Mwasipu, mawakili wa Mwanahabari, Saed Kubenea

Vilevile, Camera za CCTV pamoja na kitabu cha kumbukumbu za walinzi, vinamuonesha Makonda aliingia Clouds akiwa na askari wanne waliokuwa na sare tofauti za majeshi ya ulinzi na usalama, kati yao watatu wakiwa na silaha za moto.

Askari hao waliingia hadi chumba cha utangazaji, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za utangazaji, huku Makonda akitumia vitisho dhidi ya wafanyakazi wa Clouds kwa kutumia silaha za moto.

Kwa mujibu wa hati ya kiapo ya Kubenea, kitendo cha Makonda cha kuvamia televisheni ya Clouds, tena akiwa ameongozana na askari waliobeba silaha za moto, ni kinyume cha sheria ya Kieletroniki na Posta ya mwaka 2010.

Maombi ya kutaka kumshitaki Makonda yamewasilishwa mahakamani, chini ya kifungu cha 99 (1) cha Sheria ya mwenendo wa mashauri ya Jinai, Sura ya 20.

Kubenea ambaye amewahi kuwa mbunge wa Ubungo (Chadema), katika Bunge lililopita anasema, hatua ya Makonda kuvamia Clouds, ni matumizi mabaya ya madaraka, chini ya kifungu cha 96 ya Kanuni ya adhabu (Penal Code), Sura ya 20 na kuingilia moja kwa moja, mawasiliano ya Kieletroniki.

Mbali na Makonda, wengine walioitwa mahakamani siku hiyo, ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Wawili hawa wanadaiwa wameshindwa kuchukua za kumfungulia mashitaka ya jinai mtuhumiwa huyo.

error: Content is protected !!