September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makonda: Asanteni wana Kigamboni

Spread the love

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewashukuru wananchi wa Kigamboni jijini humo kwa kumfanya kuwa sehemu ya maisha yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Makonda ametoa pongezi hizo leo Jumanne tarehe 21 Julai 2020 ikiwa ni siku moja imepita tangu aliposhindwa kura za maoni za kuwania ubunge wa Kigamboni kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Makonda alikuwa miongoni mwa wagombea 78 waliotia nia ya kuomba ridhaa ya CCM kimpitishe kuwania ubunge wa jimbo hilo akiwemo mbunge anayemaliza muda wake, Dk. Faustine Ndugulile aliyeibuka mshindi.

Katika matokeo hayo, Makonda alipata kura 122 huku Dk. Ndugulile akipata kura 190.

Leo Jumanne tarehe 21 Julai 2020, Makonda ametumia ukurasa wake wa Instagram kuzungumzia kile kilichojitokeza kwenye mchakato wa kura za maoni.

“Nimepata pole nyingi sana kutokana na matokeo ya jana. Kwanza nawashukuru kwa upendo wenu na maombi yenu ya kunitakia mafanikio katika kutimiza ndoto yangu,” amesema Makonda

“Jambo moja Kubwa na muhimu ni kuyajua mapenzi ya Mungu na katika hili mapenzi ya Mungu ni makubwa kuliko mapenzi yangu. Nawatakia baraka na afya njema siku zote za maisha yenu.”

Makonda amemalizika akisema, “asanteni sana sana Wana KIGAMBONI kwa upendo wenu na kunipa nafasi niwe sehemu ya maisha yenu.”

error: Content is protected !!