August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makonda alitishia kuwafunga jela Clouds

Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam

Spread the love

KAMATI ya Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya kuchunguza uvamizi uliofanywa kwa studio za Clouds Media na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, imekabidhi ripoti yake leo mchana, anaandika Pendo Omary.

Katika ripoti hiyo, iliyosomwa na Mhariri Mtendaji wa Jamhuri Media, Deodatus Balile, imeelezwa kuwa imethibitishwa Paul Makonda aliingia kituo cha Clouds Media usiku wa saa 4:30 akifuatana na askari kadhaa wenye silaha za moto na kwenda moja kwa moja studio za Clouds TV ambako alitishia wafanyakazi waliokuwa wakirusha kipindi cha SHILAWADU.

Ripoti imesema Makonda alitaka kutimiziwa matakwa yake si hivyo atawafunga watangazaji kwa miezi sita jela, bila ya kuwapeleka mahakamani, na pia angewahusisha na dawa za kulevya.

Makonda alitaka kulazimisha kutangazwa habari aliyoitaka yeye ikihusu madai ya mwanamke Grace Hamis Athumani kuwa amezaa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Dk. Josephat Gwajima, baada ya kuambiwa haitarushwa mpaka ifanyiwe kazi kitaaluma.

Ripoti hiyo ilisomwa mbele ya waziri Nape ambaye baada ya kupokea alisema akishapitia atawasilisha mapendekezo kwa mamlaka ya juu yake, akitaja wakuu wake ni Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais. Alitaka mamlaka nyingine za kihabari zichukuwe hatua wanazoona zinafaa.

Kwa mujibu wa Balile, imeonekana Makonda kwa kile alichokifanya akitumia askari waliokuwa na silaha, amevunja sheria za nchi ikiwemo ya kuzuia utekelezaji wa uhuru wa habari.

Alisema pia Makonda aliwaonya wafanyakazi wa Clouds TV kuwa yote yaliyotokea ndani yabaki kuwa siri ya ofisi hiyo, na mtu atakayethubutu kuyatoa nje, “atamjua yeye ni nani.”

“Kamati imethibitisha pasi na shaka kwamba kulikuwa na vitisho dhidi ya wafanyakazi wa Clouds… askari wenye silaha za moto waliingia kibabe ndani ya studio wakiwa wameshika silaha za moto, mkuu wa mkoa aliwatisha wafanyakazi kuwa atawafunga jela miezi sita wasiporusha habari yake,” amesema Balile ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Kuhusu mapendekezo ya kamati, Balile amesema Makonda anapaswa kuwaomba radhi wafanyakazi wa Clouds Media Group kwa tukio lililotokea; pia awaombe radhi waandishi wa habari wote nchini.

Pia, Kamati imemtaka Waziri Nape apeleke taarifa kwa mamlaka juu yake ili Makonda achukuliwe hatua na vyombo vya ulinzi na usalama viwajibike kuchunguza askari walioshiriki tukio hilo kwa kuwa nao wamekiuka sheria ya matumizi ya silaha.

Aidha, kwa upande wa uongozi wa Clouds Media Group, wameshauriwa kutizama upya sera na sheria zinazosimamia habari ili kukabidhi jukumu la kuhariri habari kwa wahariri wenye ujuzi badala ya kuwaachia watu wasio wahariri kushiriki kazi ya kuhariri habari.

Kuhusu kuhojiwa kwa Makonda na Kamati hiyo, Balile amesema hakutoa ushirikiano kwani walipompigia simu hakupokea. “Hata tulipomtumia meseji hakujibu na tulipofika ofisini kwake na kumkuta, tuliambiwa kusubiri lakini aliondoka kupitia mlango wa nyuma.”

Kamati hiyo iliongozwa na Dk. Hassan Abbas, Mkurugezi wa Idara ya Habari (Maelezo). Wajumbe wengine ni Jese Kwayu, Mhariri Mtendaji gazeti la Nipashe, Neng’ida Johannes (Wapo Redio) na Mabel Masasi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

error: Content is protected !!