August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makonda akurupua ombaomba Dar

Spread the love

PAUL Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ametoa amri ya kutaka ombaomba wote jijini Dar es Salaa kusitisha kazi hiyo vinginevyo atawachukulia hatua kali, anaandika Regina Mkonde.

Amesema, ugumu wa maisha sio sababu ya ombaomba hao kuzagaa barabarani na kwamba, zipo sehemu nyingi zinazotoa msaada wa aina mbalimbali ikiwemo inayowahusu.

Makonda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi Mkoa wa Dar es Salaam amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Makao Makuu ya Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

“Watu wanaosimama katikatika ya barabara, kuomba na kufanya biashara muda wao umefika kikomo, warudi walikotoka, sababu walikuja kwa gharama zao na wanatakiwa warudi kwa gharama zao,” amesema Makonda.

Amesema kuwa, jiji hilo linapaswa kuendeshwa kwa misingi ya kanuni na sheria na si ovyo kama ilivyo sasa.

“Msako maalum utaanza Jumatatu ijayo, atakayekutwa sehemu zilizokatazwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesema.

Amsema kuwa, asilimia 80 ya ombaomba jijini Dar es Salaam wanatoka nje ya jiji hilo na asilimia 20 walikuwa wakihifadhiwa katika vituo vya misaada hivyo amewataka kwenda kwenye sehemu husika zinatoa misaada badala ya kuzagaa barabarani.

“Kuna sehemu nyingi zinatoa misaada ikiwemo makanisa, misikiti na vituo vya kutoa misaada. Wanatakiwa waende kuomba misaada maeneo hiyo, wanapojazana mjini wanachangia uchafuzi wa mazingira kutokana na kujisaidia ovyo kwenye ofisi na maduka ya watu,” amesema.

Katika hatua nyingine Makonda amewataka wamiliki wa majengo makubwa yasiyo na sehemu za kuegesha magari, kuyabomoa haraka au kulipa faini na kutafuta utaratibu wa kupata nafasi ya maegesho kama taratibu zinavyosema.

error: Content is protected !!