July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makonda ajikomba kwa Magufuli

Spread the love

PAUL Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ni mkurupukaji, mawazo na hatua anazochukua zinalenga zaidi kujipendekeza kuliko kutoa huduma, anaandika Happyness Lidwino.

Juzi Makonda alitangaza mbele ya viongozi wa vyama vya usafirishaji abiria na madereva Mkoa wa Dar es Salaam kwamba kuanzia tarehe 7 Machi mwaka huu, walimu wa Shule za Msingi na Sekondari Dar es Salaam wataanza kupanda daladala bila kulipa nauli.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni mwendelezo wa kujikomba kwa Rais John Magufuli ambaye kwenye mkutano wake na wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika wiki mbili zilizopita, alisifiwa.

Wakati walimu wakidai kwamba kupanda daladala si sehemu ya madai yao kwa serikali na kwamba ni udhalilishaji, madereva na wamiliki wa daladala hizo wamedai ‘lazima walipe kwa kuwa wanafanya kazi.’

Salim Mohammed ambaye ni Dereva wa Daladala linalofanya safari zake kutoka Kawe kwenda Buguruni amesema, hatua hizo haziakisi kuwa ni kiongozi bora na mwenye imani kwa jamii yake isipokuwa kujipendekeza.

“Ana imani na walimu lakini si madereva wa daladala wala wamiliki wake, huwezi kuwa kiongozi wa namna hiyo. Uamuzi unaoufanya lazima uzingatia pande zote mbili,” amesema Mohammed na kuongeza;

“Hawa walimu wataingia aibu tu, ni bora huyu mkuu wa wilaya akatafuta utaratibu wingine wa kuwasaidia, mbona tunasikia wana matatizo kibao lakini hawasikilizwi?”

Ezekiah Oluoch, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) anasema “wangetoa pesa na kutuwekea kwenye akaunti zetu ili tujilipie wenyewe nauli,” amesema Oluoch.

Oluoch ameonesha kushangazwa na kauli hiyo ya kutaka kupanda daladala bure na kwamba, walimu wangetatuliwa matatizo yao.

Ameonesha kuwa hakua na haja ya kutengenezwa vitambulisho vya walimu kwa ajili ya kuonesha kwenye daladala na kwamba, wao kama wadau wakuu wa sekta hiyo hawakushirikishwa.

Kutokana na hatua hiyo, amehoji kama wamiliki pia makondakta kama watakuwa tayari kutekeleza agizo hilo la Makonda “…na je, wamiliki na makonda wa daladala watakuwa tayari kutuhudumia kama wateja wa kawaida?” amesema Oluoch.

Dereva wa Daladala inalofanya safari zake kutoka Makumbusho kwenda Posta ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake amehoji sababu za walimu kwenda bure licha ya kulipwa mshahara na serikali.

“Mimi bosi anataka nipeleke pesa yake,inawezekanaje nikaanza longolongo halafu akubali. Tatizo hilo linatokana na viongozi kupenda kukurupuka na kufanya maamuzi kwa kutaka sifa,” amesema.

Akiwani miongoni mwa madereva wengi waliolalamikia hatua ya Makonda, dereva huyo amelalamika kwamba idadi ya watu wanaotaka huduma ya bure kutoka kwenye daladala inaongezeka huku akitaja polisi na wanajeshi ambao wanabebwa bila kulipa hata senti tano.

Makonda alisema wazo lake la kutaka walimu wasafiri bure limeungwa mkono na viongozi wa vyama vya wasafirishaji abiria na wamiliki wa daladala na kwamba kilichobaki ni kuanza kutoa huduma hiyo.

“Awali, wazo langu ilikuwa walimu wa Wilaya ya Kinondoni ninayoiongoza, ndiyo wafanyiwe utaratibu wa kusafiri bure lakini wadau wa usafirishaji wakashauri iwe kwa mkoa mzima. Nikamweleza mkuu wa mkoa na akaniruhusu tufanye hivyo mkoa mzima,” alisema Makonda ambaye alisifiwa na Rais Magufuli kutokana na mpango wake wa kuchangia ujenzi wa shule.

Makonda alisema baada ya Rais Magufuli kutangaza elimu bure, aliona amuunge mkono kwa kuweka mazingira yatakayorahisisha utendaji kazi wa walimu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala cha Dar es Salaam (Darcoba), Sabri Mabruki alisema wamekubali kutoa usafiri bure kwa walimu ili kumuunga mkono Magufuli katika juhudi zake za kuboresha elimu.

Hata hivyo Makonda hakujadliana na Darcoboa “tumeletewa ombi na mkuu wa wilaya akitueleza kuhusu wazo la kutaka kusafirisha walimu bure. Kwa namna Makonda na Rais wanavyofanya kazi, hatukuwa na kinyongo zaidi ya kukubali ombi hilo,” amenukuliwa Mabruki.

error: Content is protected !!