April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Makonda ‘ahaha’ kukwepa kitanzi cha JPM

Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam

Spread the love

PAUL Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amewaagiza wafanyabiashara mkoani humo, kesho tarehe 14 Oktoba 2019 kuchelewa kufungua maduka, ili wakajiandikishe kwenye orodha ya wapiga kura, katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Makonda ametoa agizo hilo leo tarehe 13 Oktoba 2019 wakati akizungumza na wanahabari, jijini Dar es Salaam.

Agizo hilo la Makonda limekuja siku moja, baada ya Rais John Magufuli kutangaza kiama kwa viongozi wa mikoa na wilaya, zitakazofanya vibaya kwenye zoezi la uandikishaji orodha ya wapiga kura,  linalomazika kesho.

Rais Magufuli alitangaza kwamba, kiongozi wa mkoa au wilaya, atakayeshindwa kuhamasisha wananchi wake kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura, atamchukulia hatua.

Kufuatia agizo hilo, Makonda amewahimiza wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kujiandikisha ili wapate haki ya kupiga kura, na kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa mwasisi wa demokrasia nchini.

“Kesho tarehe 14 Oktoba ni kumbukizi ya miaka 20 tangu Baba wa Taifa atangulie mbele za haki,na kwakuwa kesho ni siku ya mwisho ya kujiandikisha katika daftari la mpiga kura, ili kuwapata Viongozi wa Serikali za Mitaa, naelekeza maduka yote yafunguliwe saa 5 asubuhi ili tukajiandikishe,” ameagiza Makonda na kuongeza.

“Mimi kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kukuza demokrasia ndani ya mkoa wetu na nchi yetu kwa ujumla, naelekeza maduka yote yafunguliwe kuanzia saa 5 asubuhi. Kwakuwa hii ni sehemu ya kumuenzi Baba wa Taifa katika kuhakikisha wote tunajiandikisha ili kupata haki ya kupiga kura.”

Makonda amesema Mwalimu Nyerere alithamini viongozi wa serikali za mitaa, kwa kuwa ni nguzo kuu kwenye uendeshaji wa shughuli za serikali.

Wakati huo huo, Makonda amesema kesho atatembelea maeneo ya starehe, ikiwemo Bar, ili kuhamasisha wananchi wajiandikishe kwa ajili ya kupiga kura.

“Ndugu zangu wenye klabu, Bar na sehemu zote za starehe, naomba wahamasisheni watu wenu kwenye maeneo yenu kuhakikisha wamejiandikisha. Na kesho miongoni kwa maeneo nitakayoyatembelea ni pamoja na Bar, ni matumaini yangu nikifika nitakukuta ukiwa tayari umejiandikisha” amesema Makonda.

Zoezi la uandikishaji katika Orodha ya Wapiga Kura linafanyika kwa muda wa siku saba, ambapo lilianza tarehe 8 Oktoba 2019 na linatarajia kumalizika kesho.

error: Content is protected !!