May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makocha 55 wajitosa kumrithi Sven Simba

Sven Vandenbroeck

Spread the love

KLABU ya Simba ya jijini Dar es Salaam nchini Tanzania imesema, makocha 55 wametuma wasifu (CV) wakiwania nafasi moja ya kuwafundisha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa sasa, Simba inafundishwa na kocha msaizidi, Suleiman Matola, baada ya aliyekuwa kocha wake mkuu, Sven Vandenbroeck kuachana na timu hiyo kwa makubaliano ya pande zote mbili Alhamisi tarehe 7 Januari 2021.

Wakati Sven akisema, ameachana na Simba ili kumwezesha kuwa na uwiano kati yake na kazi, familia na maendeleo binafsi, jana Jumamosi, Klabu ya FAR Rabat inayoshiriki Ligi Kuu nchini Morocco, ilimtangaza Sven kuwa kocha wake mkuu kwa mkataba wa miaka miwili.

Barbara Gonzalez,Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba

Jana Jumamosi tarehe 9 Januari 2021, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alisema, wanaendelea na uchambuzi makini ili kumpata kocha bora atakaowafikisha kwenye malengo waliojiwekea na hawatokuwa na haraka kwenye mchakato huo.

Barbara alisema, wameweka masharti ikiwemo uzoefu wa kocha kwenye timu za taifa, mashindao ya Shirikisho la Soka Afrika kwa maana ya Klabu Bingwa na Kombe la Shirikisho.

“Mpaka sasa kuna walimu 55 ambao wameomba kazi. Tunaendelea na uchambuzi ili kumpata kocha sahihi kwa ajili ya timu yetu na tumekwisha kuweka masharti fulani ikiwemo uzoefu wake kwenye kazi kama timu za Taifa na mashindano ya CAF,” amesema Barbara.

Amesema, hawatakuwa na haraka ya katika kufanya uchambuzi lengo ni kumpata kocha bora ili wasije kumpata kocha ambaye anaweza “kuharibu mipango yetu ya Ligi ya Mabingwa na mashindano mengine.”

Ofisa mtendaji mkuu huyo amesema, katika kipindi chote, timu hiyo itaendelea kuwa chini ya kocha msaidizi, Suleiman Matola.

Simba kwa sasa iko visiwani Zanzibar katika michuano ya mapinduzi ikiwa imeshunda uwanjani mara mbili dhidi ya Chupukizi na kuifunga 3-1 na jana ilicheza na Mtibwa Sugar na kuifunga 2-0.

Hadi Sven anaondoka, ameiacha imefuzu hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika ikiwa imepangwa kundi A pamoja na timu za Al Merrikh (Sudan), AS Vital (DRC Congo) na Al Ahly ya Misri.

error: Content is protected !!