July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makinda azidi kuwafagia UKAWA, atimua wengine 35

Wabunge wa Upinzani wakitoka nje ya Bunge

Spread the love

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amewafukuza bungeni wabunge wengine 35 wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni baada ya kuwafukuza wengine 11 jana. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Kutokana na hali hiyo, wabunge wa upinzani waliofukuzwa kati ya juzi na jana wamefikia 46 kati ya wabunge 90 wa kambi hiyo.

Tukio la wabunge 35 kufukuzwa, lilitokea bungeni jana saa tatu asubuhi muda mfupi baada ya Spika huyo kusoma dua ya kuliombea Bunge.

Baadhi ya waliofukuzwa jana kwa upande wa Chadema ni pamoja na Ezekia Wenje (Nyamagana), Mustafa Akunay (Mbulu), Israel Natse (Karatu), Lucy Owenya (Viti Maalum), Grace Kiwelu (Viti Maalum) pamoja na Profesa Kulikoyela Kahigi (Bukombe).

Kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF), waliofukuzwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Amina Mwidau (Viti Maalum), Salum Baruani (Lindi Mjini), Musa Haji Kombo (Chakechake) na Mbunge wa Mgogoni, Kombo Hamis Kombo.

Pamoja na kuwafukuza bungeni, Spika Makinda alisema wabunge hao hawataruhusiwa kuhudhuria vikao vitano vya Bunge vilivyobaki kabla Bunge halijavunjwa wiki ijayo.

Kabla wabunge hao hawajafukuzwa jana, Wenje alisimama na kuomba mwongozo wa Spika zikiwa ni dakika chache kabla Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawe, hajawasilisha kwa hati ya dharura miswada mitatu inayopingwa na wabunge hao.

Miswada hiyo ni Muswada wa Sheria ya Petroli wa Mwaka 2015, Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015 na Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji Katika Tasnia ya Uchimbaji Tanzania wa Mwaka 2015.

Katika mwongozo wake, Wenje alihoji ni kwa nini askari wa Bunge walimzuia kuingia bungeni jana, Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema) wakati jina lake haliko kwenye orodha ya wabunge waliozuiwa kuhudhuria vikao vya Bunge kuanzia juzi.

Aidha, alitaka kujua ni kwanini Serikali inataka kuwasilisha bungeni miswada mitatu inayohusu masuala ya petroli, gesi na mafuta kwa hati ya dharura wakati miswada hiyo imekataliwa na wabunge pamoja na wadau wa sekta ya nishati nchini.

Akijibu mwongozo huo, Spika Makinda alisema Mbunge Silinde ni kati ya wabunge waliofungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge kuanzia juzi kwa kuwa alishiriki kufanya fujo juzi.

“Silinde hatakiwi kuhudhuria na kama hakutajwa katika orodha jana (juzi), jina lake lilisahaurika tu kwa sababu naye nilikuwa nimemtaja.

“Kuhusu miswada mitatu kuwasilishwa kwa siku moja, hakuna kanuni iliyokiukwa na wanaolalamikia hilo, hawajui kanuni zinasemaje ingawa wamekaa bungeni kwa muda mrefu,” amesema Spika Makinda.

Baada ya kusema hivyo, Wenje alisimama na kuanza kumlalamikia Spika akisema anawaonea wabunge wa upinzani kwa kuwa anaipendelea Serikali.

“Mheshimiwa Spika unatuonea, Silinde hakutajwa katika orodha ya waliozuiwa kuingia bungeni na kama jina lake lilirukwa kama unavyosema, wewe huna mamlaka ya kumzuia kuingia hapa kwa mujibu wa kanuni za Bunge hadi upate mapendekezo ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge,” alilalamika Wenje.

Kauli hiyo ilionekana kumkera Spika kwani alisimama na kutishia kumfukuza bungeni Wenje kwa kile alichosema anavunja kanuni za Bunge na mvutano kati yao ulikuwa hivi.

Spika: Wenje naona unatumia delaying tactics, kama hutaki kutulia utaondoka hapa kwa sababu nimeshakwambia jina la Silinde lilirukwa tu lakini hatakiwi kuwa hapa.

Wenje: Usitake kutumia vitisho, mimi siwezi kuogopa kufukuzwa kwa sababu haitakuwa mara ya kwanza kufukuzwa hapa.

Spika: Wenje unaongea bila kufuata utaratibu itabidi sasa utolewe nje.

Wenje: Mheshimiwa Spika, nakwambia unatuonea, sijawahi kuona Bunge lolote duniani likiwasilisha miswada mitatu kwa wakati mmoja, wewe tuonee tu.

Spika: Sasa nasema Wenje atolewe nje na hatahudhuria vikao vitano kuanzia sasa.

Spika alipotoa uamuzi huo, Wenje alitoka nje akiongozwa na askari wa Bunge huku wabunge wote wa Kambi ya Upinzani wakiwa wamesimama na kuanza kupiga kelele wakitaka wafukuzwe wote.

Kauli hiyo ilimsimamisha tena Spika na kuwaambia wabunge hao. Kama mnataka kufukuzwa endeleeni kusimama ili niwaandike majina baadaye niwafukuze.

Spika aliposema hivyo, wabunge hao walisema kwa pamoja, tutasimama, tuandike vizuri.

Baada ya hapo, maofisa wa Bunge walianza kuandika majina hayo na kisha walimkabidhi orodha hiyo Spika Makinda ambaye aliisoma na kuwafukuza bungeni akitumia kanuni ya Bunge ya 74 (1).

Kutokana na uamuzi huo, miswada hiyo iliwasilishwa kwa mujibu wa ratiba ya Bunge kisha wabunge waliichangia.

Sakata la wabunge kupiga miswada hiyo, lilianza Juni 29 mwaka huu wakati wabunge wote walipokutana na wadau wa sekta ya nishati kujadili miswada hiyo mjini hapa.

Wakati wa semina hiyo, wabunge wa upinzani na CCM waliungana kuipinga miswada hiyo ambapo Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage, alimrushia maneno ya kashfa Mbunge wa Igunga, Dk. Dalaly Kafumu (CCM) baada ya mbunge huyo kuikataa miswada hiyo.

error: Content is protected !!