Monday , 30 January 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Makamu wa Rais ataka ushirikiano kupambana na mabadiliko ya tabianchi
Habari Mchanganyiko

Makamu wa Rais ataka ushirikiano kupambana na mabadiliko ya tabianchi

Spread the love

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuwa tishio na changamoto kubwa hapa Visiwani, kutokana na athari za moja kwa moja katika maisha ya wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Othman ameyasema hayo leo tarehe 25 Januari 2023 Ofisini kwake Migombani Zanzibar, akizungumza na Naibu Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Rick Shearn, kuhusu masuala mbalimbali ya mazingira, ushirikiano, uchumi, jamii na maendeleo.

Amesema tishio na changamoto zaidi za mabadiliko ya tabianchi, zinadhihiri katika mwenendo mzima wa maisha ya kawaida ya wananchi na hasa wanaoishi katika ukanda wa pwani ambako kwa kiasi kikubwa kumebainika athari za waziwazi.

Akitaja viashiria vya athari hizo, Othman ameeleza hali ya maeneo mengi ya visiwa vya Zanzibar, yakiwemo ya kilimo na makaazi ya watu, kuvamiwa na maji chumvi, na hivyo kudhoofisha mavuno, kipato cha wananchi, na hatimaye kuyumba kwa uchumi, kuanzia kwa mtu binafsi, familia na ikibidi hata pato la nchi.

“Bila shaka juhudi kubwa zinahitajika na mashirikiano ya pamoja ili kunusuru hali hiyo isiendelee, kwani inaathiri hata Mipango ya Serikali kuwaletea wananchi maendeleo, ikiwemo utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Buluu”, amesema Othman.

Aidha, Othman ameeleza matumaini ya Zanzibar kupitia mahusiano mema na jamii ya kimataifa, katika kukabiliana na athari za tishio hilo kwa haraka, hasa wakati huu ambao mazingira ya kisiasa nchini yameanza kufunguka, sambamba na juhudi za kuendeleza maridhiano kufuatia uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) Visiwani humo.

Naye Balozi Shearn amesema nchi yake ipo tayari kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika utekelelezaji wa mikakati muhimu ya kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabianchi, ili hali hiyo ambayo kwa sasa ni tatizo la ulimwengu, isiendelee kuleta athari zaidi.

Balozi Shearn amesisitiza haja ya kuendelea na ujenzi wa demokrasia, utawala wa sheria na maridhiano ya kisiasa, ili kuweka mazingira bora yatakayopelekea fursa nyingi za kujiletea maendeleo na hatimaye kuijenga nchi kiuchumi.

Katika msafara wake, Balozi Shearn aliambatana na Maafisa mbalimbali kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania akiwemo Mkuu wa Masuala ya Mazingira na Tabianchi, Catherine Pye.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chongolo asikitishwa na mradi wa Mil 900 kutoanza kutoa manufaa

Spread the loveKATIBU mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo...

Habari Mchanganyiko

Huawei Tanzania yatajwa miongoni mwa waajiri bora kimataifa

Spread the loveKAMPUNI ya Huawei Tanzania imetajwa kuwa mwajiri bora nchini na...

Habari Mchanganyiko

Waziri wa uchumi wa Finland atua nchini, kuteta na mawaziri 7

Spread the loveWAZIRI wa Masuala ya Uchumi wa Finland, Mika Tapani Lintilä...

Habari Mchanganyiko

Asimilia 79 wafeli somo la hesabu matokeo kidato cha nne

Spread the loveWATAHINIWA wa shule 415,844 sawa na asilimia 79.92 ya watahiniwa...

error: Content is protected !!