May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makamu wa Rais akumbushia mapito Z’bar asema chama ni taasisi

Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar, Othman Masoud Othman ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo, amezindua kadi za ngome ya wanawake

Spread the love

 

MAKAMU wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Mapinduzi – Zanzibar, Othamn Masoud Othman ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati kuu ya ACT Wazalendo amewaomba wanachama wa chama hicho kusimama na kusonga mbele wakiwa imara licha ya mapito na mazingira magumu ya kisiasa waliyopitia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Pia amewaonya wanachama hao kusimamia chama hicho katika misingi ya kitaasisi kwa sababu chama ni taasisi na wasikubali chama kuwa jumuiya.

Othman ametoa kauli hiyo leo tarehe 26 Januari, 2022 wakati akizindua rasmi kadi ya ngome ya wanawake mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema ujio wa kadi hizo za ngome ya wanawake ni mtaji na nyenzo nyingine za kufanya kazi ndani ya chama hicho.

“Mapito tuliyopita bahati mbaya yametufanya mazingira yetu ya kufanya kazi kuwa magumu sana. Lakini lazima chama kiendelee, chama kijengwe, program za chama ziendelee, vikao vya kikatiba viendelee… kwa sababu ndio kujenga taasisi huko.

“Lazima tutambue kuwa chama ni taasisi tusikubali chama kikawa jumuiya, chama ni taasisi maana yake kina misimamo yake na tudumishe huo utaasisi,” amesema.

Amesema hata wahenga walisema; ‘Ukiona vyaelea vimeundwa’, hivyo ujio wa kadi hizo ni mwendo mpya wa kuimarisha chama hicho.

“Kama kawaida akina mama mmetuonesha njia, ya kwamba ni wabunifu wa mambo haya na hakika mmeonesha usimamizi, utekelezaji na ufanikishaji uliosheheni ufanisi wa hali ya juu. Kwa hili nawapongeza kwa dhati,” amesema.

Amesema mtaji mkubwa wa chama hicho na vyama vyote nchini ni wanachama lakini katika wanachama hao mtaji mkubwa ni wanawake.

“Katika harakati hizi tunaona maneno ya bwana mmoja aliandika kitabu kwamba katika kipindi cha miaka 2020-2030 kwamba dunia itaongozwa na wanawake. Itoshekusema name nitashabihisha kuwa nguvu ya akina mama ni kubwa.

“Niwaombe wanawake wote na viongozi wote tulione hili na tulisimamie kwa dhati kwani ndio mwelekeo wa chama chetu,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, kiongozi huyo ametoa kiasi cha Sh milioni mbili fedha taslimu kwa ajili ya kuwanunulia akina mama wa ngome hiyo ambao ni wazee kadi hizo maalumu za kielektroniki.

“Kwa hiyo mmenipa zawadi ya koti ni dalili ya mapenzi na mimi nawapa zawadi. Naomba niwanunulie akina mama wazee wa chama chetu kadi za Sh milioni mbili,” amesema.

Aidha, Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Ngome hiyo ya Wanawake wa ACT Wazalendo, Pavu Abdallah amesema kadi hizo maalumu za kielektroniki zitakisaidia chama hicho kupata idadi sahihi ya wanachama wake akina mama ambao ndio wajenzi muhimu wa chama kuwa taasisi.

Amesema zoezi hilo la ugawaji wa kadi hizo za kielektrtoniki lilianzia katka Visiwani Zanzibar na sasa ni zamu ya mkoa wa Dar es Salaam kisha kuelekea katika mikoa mingine.

error: Content is protected !!