January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makampuni 500 ya China kuwekeza Tanzania

Wafanyakazi kutoka Shirika la Mafuta la China wakikagua bomba la gesi-Mtwara Tanzania

Spread the love

MAHUSIANO ya kibiashara kati ya Tanzania na China yamechukua muelekeo mpya, ambapo makampuni 500 ya China yakitarajiwa kuanzishwa ndani ya miaka 5. Anaandika Benedict Kimbache … (endelea).

Chini ya mpango huu, Tanzania itakuwa kitovu cha viwanda vya China, huku viwanda 100 vikitegemewa kuanzishwa kwa mwaka.

Hii itaongeza bidhaa zinazozalishwa viwandani, sekta ambayo kwa sasa ndio inaongoza kwa kuingiza fedha za kigeni.

Mpango huu wa China utaongeza mapato ya nje kutoka kwenye sekta hii. Kwa mujibu wa takwimu kutoka Benki Kuu ya Tanzania, robo ya kwanza ya 2014, sekta hii ilikuwa ya kwanza kwa kuingiza fedha za kigeni, ikiipiku sekta ya madini, utalii na kilimo.

Katika robo ya nne, bidhaa za viwandani ziliongezeka kwa asilimia 25 ukifananisha na madini yaliyoshuka kwa asilimia 19.

Abdulrahaman Shimbo, Luteni Generali mstaafu na Balozi wa Tanzania nchini China amesema uwekezaji huo ni habari njema kwa Tanzania.

”Hii ni alama ya kukua kwa uhusiano wa nchi hizi, kuja kwa viwanda hivi ni changamoto kwa Tanzania kwani tunahitaji mazingira wezeshi kuweza kukaribisha viwanda hivi,”Shimbo amesema.

Mamlaka ya Maeneo Huru ya Biashara (EPZA) imeshapewa maelekezo ya kuandaa ujio wa viwanda hivyo na utekelezaji umeshaanza.  

Mbelwa Kairuki- Balozi na Mkurugenzi wa Asia na Australia wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Uhusiano wa Kimataifa, amesema Watanzania walio wengi wanaelewa visivyo kwamba Tanzania itafaidika kidogo kutoka China.

Kairuki amesema mwaka 2014, biashara kati ya nchi hizi zote ilifikia dola za Marekani bilioni 3.7 (trilioni 6.1) na Watanzania 6,000 walienda China kufanya biashara.

”Mwaka huo, Tanzania iliweza kuvutia mitaji binafsi zaidi ya dola bilioni 2.5 na mikopo kutoka China ilifikia dola bilioni 1.9”.

”Mara baada ya bandari ya Bagamoyo kukamilika na reli ya kati pamoja na Tazara kuunganishwa na bandari hii, nina uhakika Tanzania itakuwa ni kituo chenye mfumo wa viwanda,” amesema.

Stadi iliyofanyika siku za karibuni na Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umasikini (Repoa), inaonyesha kuwa Watanzania wanaamini kuwa ushawishi wa kiuchumi na kisiasa wa China kwa Tanzania una lengo zuri.

Watanzania walisema kuwa China ina ushawishi zaidi ukifananisha na Uingereza, Marekani, India, Afrika ya Kusini na taasisi za kimataifa kama Benki ya Dunia.

Utafiti huo unaonyesha Watanzania wengi zaidi wanapendelea China kuwa mfano wa kuweza kuiletea Tanzania maendeleo zaidi kwa asilimia 35, ukifananisha na Marekani (30), Afrika Kusini (100, Uingereza (6) na India (4).

Mwaka uliopita China ilichagua nchi tatu za Afrika (Tanzania, Ethiopia na Msumbiji) kama vitovu vya mipango ya uwekezaji katika bara la Afrika.

Nchi hizi tatu zitakuwa mfano wa uwekezaji wa China katika Afrika, pia zitakuwa sehemu za mfano wa kujifunza kwa nchi nyingine za Afrika. Lengo hapa ni China kuweka mkazo kwenye nchi chache za Afrika kuliko kuwekeza katika kila nchi.

error: Content is protected !!