June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makamba: Nitamaliza matatizo ya msingi ya Watanzania

January Makamba, Waziri wa Nishati na Madini

Spread the love

JANUARY Makamba, mtoto wa katibu mkuu mstaafu wa CCM, Luteni Yusufu Makamba, ameingia katika orodha ya wasaka urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akija na kauli kuwa urais kwake si mapambano na mtu yeyote. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Katika tangazo alolitolea kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam leo, Makamba amesema kutafuta kwake wadhifa huo wa juu kabisa nchini, ni kwa nia njema ya kusaidia Watanzania kuondokana na matatizo ya msingi yanayoathiri maisha yao.

Makamba, kada wa CCM, aliyezaliwa 28 Januari 1974, ni mbunge wa Bumbuli, mkoani Tanga, na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Ameendesha mkutano wake huo kwa njia ya mtandao, akiunganisha ukumbi huo na mikoa kadhaa nchini. Baadhi ya walioko nje ya ukumbi, walipata fursa ya kumuuliza maswali.

Amesema akipata ridhaa ya chama na akichaguliwa, ataunda serikali ndogo yenye mawaziri 18 tu, idadi tofauti na serikali ya Rais Jakaya Kikwete, mwanasiasa aliyemchukua Makamba kumsaidia kampeni zake za urais mwaka 2005 na alipounda serikali, akamteua mwandishi wake wa hotuba.

Dhamira yake kuu katika kuongoza serikali itakuwa ni kuhamasisha “uwezeshwaji mpana wa wananchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.”

“Badala ya kuwaahidi Watanzania kwamba tutawafanyia kila kitu, serikali nitakayoiunda itawajengea uwezo na nguvu ya maamuzi kiuchumi… waishi wapi, wapeleke watoto shule wapi, wafanye biashara gani, wajenge nyumba za aina gani,” amesema Makamba.

Makamba amesema serikali chini yake itaanzisha mfuko maalum utakaolenga kuwawezesha wananchi katika kuanzisha na kukuza biashara ndogo na za kati.

Ametambua mchango wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ambayo itakuwa dira yake, lakini akasema ana mambo ya ziada anayofikiria yana umuhimu kwa Watanzania kipindi hiki.

Ni hapa anaorodhesha vipaumbele vitano: Mosi, kukuza kipato cha watu akiamini kuwa mtu yeyote anayetumia jasho lake kutengeneza maisha yake lazima anufaike na jasho hilo; uhakika wa huduma za jamii zilizo bora zikiwemo maji, umeme, simu, afya, barabara na miundombinu mbalimbali.

Vipaumbele vingine ni kuimarisha utawala bora katika uendeshaji serikali akilenga kudhibiti ufisadi katika sekta ya umma; usimamizi wa uchumi unaozingatia haja ya kuivusha Tanzania kuwa na uchumi tajiri kwa kutegemea zaidi raslimali za ndani ya nchi.

Makamba amezungumzia pia katika kuendesha serikali, atajenga maridhiano ya mahusiano kati ya Wakristo na Waislamu kupitia asasi za makundi hayo makubwa zaidi ya dini nchini.

Katika kukuza pato la taifa, Makamba amesema atasimamia upanuzi wa wigo wa kodi zinazosimamiwa na taasisi za serikali kuu na zile za halmashauri za wilaya, majiji, miji na manispaa.

Makamba amesema amebuni mpango mahsusi wa kuongeza mapato serikalini, akitaja upunguzaji wa misamaha ya kodi kufikia asilimia 1 ya pato la taifa, badala ya tatu inayotumika sasa. Kupitia mkazo huo, amesema serikali itaingiza hadi Sh. 780 bilioni kwa mwaka.

Amegusia utalii, moja ya sekta kuu za kiuchumi nchini, akisema ataiimarisha kwa kutangaza kwa ufanisi vivutio vya utalii na kudhibiti mapato yaingie serikalini badala ya sehemu kubwa kuishia kwa kampuni binafsi za uwakala. Ameahidi kukusanya hadi Sh. 30 trilioni kutoka Sh. 3 trilioni za sasa kwa mwaka.

Atasimamia barabara ukusanyaji mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuongeza ufanisi kwa asilimia 10, hatua itakayoipatia serikali Sh. 620 bilioni kwa mwaka kama ongezeko.

Makamba hakuacha kugusa tatizo la rushwa. Amesema atajenga upya taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa ili ipate meno ikiwemo kushitaki, tofauti na ilivyo sasa, taasisi hiyo ikiendelea kulalamika kuwa kesi zake nyingi zinakwamishwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

“Kesi za kuhujumu uchumi zitaendeshwa kwa uwazi, mtumishi wa serikali akitajwa kwenye ripoti ya ubadhirifu atasimamishwa siku hiyohiyo na kesho yake hatua za kimahakama zitafuata,” amesema, huku akiahidi kuanzisha mjadala mpana katika jamii kuhusu maadili mema nchini.

Makamba amesema serikali itasimamia vizuri sekta ya ufugaji nyuki na uvuvi kwa lengo la kuwezesha wafugaji kupata mapato zaidi pamoja na kodi serikalini.

error: Content is protected !!