December 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makamba aanika mikakati kutekeleza maagizo ya Samia kuhusu nishati safi

Spread the love

KATIKA kuhamasisha Watanzania kuachana na nishati chafu ya kupikia na kuhamia kwenye nishati safi, Waziri wa Nishati, Januari Makamba amesema kwa mwaka huu wa fedha Serikali imetenga kiasi cha Sh bilioni 23 kutekeleza mpango wa kusaidia kufikisha nishati bora ya kupikia vijijini. Anaripoti Gabriel Mushi, Dar es Salaam … (endelea).

Pia amesema ndani ya miezi mitatu watahuisha mpango kabambe wa matumizi ya nishati ya gesi asilia inayozalishwa mkoani Mtwara ili kuweka mazingira ya sekta binafsi kuwekeza kwenye gesi hiyo itakayosambazwa kwa matumizi mbalimbali ikiwamo nyumbani na viwandani.

Makamba ametangaza mikakati hiyo juzi jijini Dar es Salaam katika kilele cha kongamano la Mjadala wa Kitaifa kuhusu Nishati Safi ya kupikia lililofunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kufanyika kwa siku mbili.

Akifungua kongamano hilo Rais Samia alitoa maagizo kwa viongozi wa Serikali akiwamo Waziri Makamba kuhakikisha Watanzania wanaachana na nishati chafu ya kuni na mkaa na kuanza kutumia nishati safi kama ya gesi kupikia.

Aidha, akitoa hotuba ya kufunga mjadala huo, Makamba alisema Mkuu wa nchi akishatoa maagizo, kinachofuata kwa viongozi wa serikali ambao ni maofisa wake ni kuanza kutekeleza.

 

“Kipimo chetu cha uadilifu ni utii ni kutekeleza maagizo yake, na tumeagizwa serikali nzima” alisema Makamba na kuongeza wamepata hamasa kubwa kutokana na uungwaji mkono kisiasa.

Kuhusu agizo la uundwaji wa kikundi kazi, Makamba alisema jana angelipeleka dodoso au mapendekezo kwa Waziri mkuu, Kassim Majaliwa  kuhusu muundo, utaratibu wa kazi, washiriki wa kikundi kazi hicho.

Kuhusu kuanzishwa kwa mfuko wa nishati safi ya kupikia, Makamba alisema katika kuanza kazi hiyo mapema tayari Rais alitoa ahadi ya kibajeti na wao wizara watatumia fursa mbalimbali za kupata fedha ili uanze kufanya kazi.

Agizo kuhusu taasisi kubwa kutumia nishati safi kupikia, Makamba alisema tayari amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuunda kamati itakayofanya kazi ya kuorodhesha taasisi zote za binafsi na za serikali zenye watu zaidi ya 300 ili kuziandalia mpango wa kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Tutaweka kanuni kwa sababu sheria ya mazingira katika kipengele cha 16 kinasema waziri anaweza kuweka maelekezo yoyote na hayatapingwa. Tutatumia nguvu kidogo kutekeleza hiki kitu,” alisema.

Aidha, alisema katika mambo ambayo hayatasubiri kikundi kazi hicho, ni pamoja na kufanya utafiti wa kina kuhusu hali halisi ya nishati ya kupikia nchini hasa ikizingatiwa baadhi ya wachangiaji wa mjadala huo waliitaka wizara kuandaa takwimu sahihi za nishati ya kupikia.

“Baada ya miezi mitatu ijayo tutafanya utafiti wa kina kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya na pesa ipo, kikundi kazi kitakapoanza kazi kitapata ushahidi wa takwimu kwamba Gairo wanakata miti kwa kiasi gani na miti gani,” alisema.

Mbali na kuhuisha mpango kabambe wa matumizi ya gesi asili ya Mtwara hasa ikizingatiwa kumekuwa na maneno kwanini gesi hiyo haitumiki, amesema mpango mwingine ni kukaa na wadau hususani wa taasisi za kifedha kupitia biashara ya bima au mita kuhamasisha matumizi ya gesi ya mitungi ya kupikia inayotoka nje maarufu kama LPG.

Mpango mwingine alisema kupitia Wakala wa nishati vijijini (REA) wamekuja na mpango wa kusaidia kufikisha nishati bora ya kupikia vijijini tumetenga Sh bilioni 23 zikitoka serikalini na ufadhili kutoka Benki ya Dunia (WB).

Alisema pesa hizo ambazo zimegawanywa katika makundi matatu, watashirikiana na TPDC, kusambaza gesi ambapo mikoa ya Lindi na Pwani itashiriki katika mpango wa majaribio ambao watasambaza mitungi 100,000 ya LPG.

 MONGELA: HAKUNA BABA ANAYETAKA MWANAMKE ANAYENUKA MOSHI

Awali Mwanasiasa mkongwe na mwanaharakati wa masuala ya wanawake, Balozi Getrude Mongella alitoa wito kwa wanawake kujikomboa kutoka kwenye matumizi ya nishati chafu ya kupikia na kuhamia kwenye nishati safi kwa kuwa hakuna mwanaume anayemtaka mwanamke anayenuka vumbi au moshi wa kuni na mkaa.

Alisema hana wasiwasi na wanaume kuunga mkono ajenda ya matumizi ya nishati safi na ya kupikia kwani wao pia wanataka wanawake wakomboke na kurudi kwenye maisha ambayo yataimarisha uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Akichangia mada katika kongamano la Mjadala huo alisema kwa kuwa Tanzania ilikabiliana na matatizo mengi na kufanikiwa kuvuka, pia kwenye kuachana na nishati chafu itafanikiwa kuvuka.

“Akina baba hawana tatizo katika kuunga mkono hili kwa sababu hakuna baba anayetaka mwanamke aje kitandani akiwa ananuka moshi, vumbi.. Na wao akina baba wanataka wanawake tukomboke…turudi katika maisha ambayo yataimarisha uchumi wa Taifa letu,” alisema.

Balozi Getrude Mongella

Alisema kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi kuwa wawaondoe wanawake katika madhara wanayopata kwa kutumia nishati chafu, hakuna yeyote anayepaswa kukataa kutekeleza maagizo hayo.

Aidha amesema katika uchaguzi ujao mbunge atapata kura kulingana na idadi ya mitungi ya gesi aliyowagawia wananchi wake badala ya khanga na vikombe vya kunywea gongo.

Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Prof. Romanus Ishengoma aliishauri Serikali kujiridhisha na umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na iwapo imejipanga kukabili madhara yanayoweza kujitokeza ya watu kukosa ajira na kufa kwa viwanda vidogovidogo vya uzalishaji nchini.

“Ninawachokoza na hoja zangu je, unataka tuhamie kwenye gesi ni sawa lakini kuhama huku unaharibu ajira za watu wangapi, na baada ya hapo watu hawa watafanya nini na je, nishati safi ya kupikia ni ipi haya ni mambo ya msingi ya kujiuliza,” alihoji.

error: Content is protected !!