November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama EACJ hapatoshi: Mbowe, Maalim Seif, Zitto ndani

Spread the love

KESI ya kupinga sheria mpya ya vyama vya siasa nchini, imeanza kusikilizwa leo tarehe 19 Juni 2019, jijini Arusha ambapo miamba mitatu kutoka vyama vya upinzani wamehudhuria. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa; Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo na Maalim Seif Sharif Hamad, Mshauri Mkuu wa ACT-Wazalendo ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa waliohudhuria kesi hiyo leo.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Dk Faustine Ntezilyayo kutoka nchini Rwanda, Jaji Monica Mugenyi wa Uganda, Fakihi Jundu kutoka Tanzania, Jaji Dk. Charles Nyawelo kutoka Sudani Kusini na Charles Nyachai wa nchini Kenya.

Upande wa mashtaka unataka mahakama hiyo isitoshe utekelezwaji wa sheria hiyo, hasa kipindi hiki kuelekea chaguzi mbalimbali kwa madai kuwa, sheria hiyo inakiuka Katiba ya Jamhuri.

Kwenye kesi hiyo, viongozi hao wa upinzani wanaongozwa na Wakili John Mallya, Fatuma Karume na Jebra Kambole. Mbele ya majaji hao Fatma Karume amewaeleza kuwa, sheria hiyo inakiuka mkataba wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki hususani kwenye haki na demokrasia.

Akitaja udhaifu kwenye sheria hiyo Fatma amesema kuwa, sheria hiyo inazuia viongozi wa kisiasa kutoa elimu ya mpiga kura isipokuwa lazima wapate kibali kutoka kwa msajili wa vyama vya siasa.

Sababu nyingine kati alizozieleza mahakama hiyo ni kwamba, sheria hiyo inazuia walinzi binafsi wa vyama vya siasa jambo ambalo linaingilia uhuru wa vyama.

Hata hivyo, majaji hao wameahirisha kesi hiyo kwa muda kwa lengo la kufanya majadiliano iwapo waendelee kusikiliza kesi upande mmoja wa walalamikaji ama kuishirikisha serikali.

error: Content is protected !!