January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makaidi akaidi UKAWA

Spread the love

MWENYEKITI wa National League for Democracy (NLD), Dk. Emmanuel Makaidi ameshikilia kuendelea na kampeni ya kugombea ubunge jimbo la Masasi mkoani Mtwara, licha ya wananchi kueleza wazi watamchagua Ismail Mapembe (Kundambanda) wa Chama cha Wananchi (CUF).Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Dk. Makaidi ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa wenyeviti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), amesema anabaki jimboni kwa sababu hilo ni moja ya majimbo matatu ambayo NLD imepata katika mgao wa majimbo ya kugombea.

Majimbo mengine mawili ambayo chama hicho kilichosajiliwa mwaka 1992 mara baada ya mfumo wa vyama vingi kurudishwa nchini, ni Ndanda anakogombea Angolaus Thomas, na Lulindi, yote ya mkoani Mtwara.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu mara baada ya kukamilisha mkutano wa kampeni jana, Dk. Makaidi amesema anajua Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutaka kuwachanganya UKAWA ili wazigawanye kura na kuibuka wao washindi.

Mtafaruku wa ugombeaji ubunge Masasi umetanuka baada ya wananchi kudhihirisha wanavyomtaka Kundambanda walipoulizwa na Edward Lowassa, anayegombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwakilisha UKAWA.

Lowassa alipohutubia mkutano wa kampeni Masasi mjini Jumatano wiki iliyopita, aliwauliza wananchi katika hali ya kutoelewana jimboni kwa kuwapo wagombea wawili, ni yupi watamchagua, na wakajibu wanamuunga mkono Kundambanda.

Lowassa aliwaita wote wawili, akataka wahutubie wananchi, walipomaliza akainua mikono yao kulia na kushoto kwake, akauliza “mnataka yupi.” Walijibu Kundambanda.

Lowassa alipoona hivyo, alimgeukia Dk. Makaidi na kumwambia angeachia kugombea na asubiri kupewa kazi nyingine ya kufanya. Hata hivyo, Dk. Makaidi kuonesha kutoridhika, aliondoka kwenye mkutano.

Kampeni yake imekuwa ikitatizwa na wananchi kwa kuonekana anadhoofisha nguvu ya UKAWA kushinda ubunge Masasi.

error: Content is protected !!