December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Makada wa Chadema waliofungwa maisha waachwa huru baada ya kusota miaka 2

Spread the love

MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Shinyanga, imewaacha huru wanachama wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Katala Kikaja na Ng’hulima Lilanga, baada ya kushinda rufaa yao dhidi ya adhabu ya kifungo cha maisha walivyohukumiwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Shinyanga … (endelea).

Kikaja na Lilanga, walihukumiwa kifungo cha maisha baada ya kuitwa hatiani kwa makosa ya wizi, unyang’anyi wa kutumia silaha na ubakaji.

Wanachama hao wameachiwa huru leo Jumatano, tarehe 16 Novemba 2022 na mahakama hiyo baada ya Jaji Mfawadhi, Athumani Matuma, kutoa uamuzi wa rufaa ya jinai Na. 46/2022 waliyokata, kupinga hukumu ya kutumikia kifungo cha maisha, iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, katika kesi ya jinai Na. 142/2020, iliyokuwa inawakabili.

Akitoa uamuzi wa rufaa hiyo, Jaji Matuma alisema, katika kesi ya msingi iliyokuwa inawakabili wanachama hao, upande wa Jamhuri ulishindwa kuleta mashahidi muhimu, kitendo kilichosababisba ushahidi wao kutoaminika na kukosa nguvu.

Jaji Matuma amesema, hakimu aliyewahukumu kifungo cha maisha warufani hao, hakufuatilia kwa kina ushahidi na kwamba aliwatia hatiani kwa ushahidi wenye shaka.

Wanachama hao wa Chadema wameachwa huru baada ya kusota rumande kwa zaidi ya miaka miwili, tangu walipokamatwa siku ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020.

Katika kesi ya jinai iliyokuwa inawakabili, Kikaja na Lilanga walikuwa wanashtakiwa kwa makosa matano, likiwemo la genge la ubakaji, wizi, unyang’anyi wa kutumia silaha, waliyodaiwa kutenda tarehe 28 Oktoba 2020 katika Kituo cha Kupigia kura kilichokuwepo kwenye Shule ya Msingi Tunge, wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu.

Wanachama hao wa Chadema, walidaiwa kufanya makosa hayo kwa watu kadhaa ikiwemo aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi wa kituo hicho, wakishinikiza kutangazwa kwa matokeo halisi baada ya kupinga matokeo ya ubunge na udiwani, yaliyowapa ushindi wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

error: Content is protected !!