January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majokofu hospitali M’nyamala kukaguliwa

Spread the love

MAJOKOFU ya kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mwananyamala, yaliyoharibika kwa zaidi ya wiki mbili yanatarajiwa kufanyiwa ukaguzi kesho, baada ya matengenezo yaliyofanyika juzi. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Katibu Afya wa hospitali hiyo, Willborada Athanase amesema majokofu hayo yaliharibika kwa muda wa wiki mbili na kusimamisha shughuli za uhifadhi maiti, lakini tayari yamemkamilika baada ya kufanyiwa matengenezo.

Athanase amesema kesho wanatarajia kuyafanyia ukaguzi ya majokofu hayo kabla ya kuanza kuyatumia tena kwa kuhifadhia maiti kutoka ndani na nje ya hospitali hiyo.

Athanase amesema kuwa hitilafu za majokofu hayo zilitokana na uchakavu huku mara kadhaa kushindwa kufanya kazi wakati mahitaji ya kuhifadhi miili yakiongezeka.

Amesema wananchi wasiwe na hofu kwakuwa tatizo hilo limeshapatiwa ufumbuzi, hivyo mara baada ya kufanya ukaguzi huo kesho watatoa taarifa kwa umma juu ya kuanza kupokea na kuhifadhi miili kutoka nje ya hospitali.

Kwa mujibu wa Katibu huyo, hospitali ya Mwananyamala ina jumla ya majokofu matano yenye uwezo wa kuhifadhi maiti tatu kwa kila moja, lakini manne yalikuwa na hitilafu huku moja likiendelea kutumika kwa kuhifadhi maiti kutoka ndani ya hospitali hiyo.

Mmoja wa wananchi waliofika katika hospitali hiyo jana kwa lengo la kuhifadhi maiti ya ndugu yake, ilishindikana na kulazimika kuupeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Daud Michael amesema hitilafu hiyo imeleta usumbufu kwa wananchi wasiokuwa na taarifa za ubovu wa majokofu hayo.

Michael amesema kuwa kuharibika kwa majokofu hayo kumepelekea gharama za kusafiri mara mbili, kutokana na kukosa taarifa za ubovu wa majokofu hayo.

“Suala hili limepelekea watu wamekuwa wakija na maiti kisha wanaambiwa kuwa majokofu hayafanyi kazi, inabidi kuingia gharama tena ya kwenda Muhumbili,” anasema Michael na kuongeza:

“Sekta kama hizi muhimu ziwe na utaratibu wa kutoa taarifa na si taarifa pekee na ufafanuzi wa suala husika kwa njia ambazo wananchi wanaweza kuzifikia kiuwepesi.”

error: Content is protected !!