January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majipu yasababisha Rais Magufuli aongezewa ulinzi

Spread the love

MAASKOFU Mkoani Dodoma wamewaomba Watanzania kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli kwa lengo la kumuongezea ulinzi ili aendelee kuisafisha nchi ambayo iligubikwa na harufu ya ufisadi, rushwa pamoja na kutokuwajibika kwa watendaji wake. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Mjini hapa kwa nyakati na Maaskofu katika ibada ya kumbukumbu ya kuzaliwa wa Yesu Kristo.

Askofu, Amos Kinyunyu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Dodoma, amewataka Watanzania kuzidi kumuombea Rais Dk. Magufuli kutokana na utendaji kazi wake unaowagusa Watanzania wa hali ya chini.

Alisema wao kama kanisa wataendelea kumuombea ili aweze kufanya kazi  anayoendelea kufanya sasa hivi kwani hata vitabu vitakatifu vinataka usawa katika uchumi wa kipato kwa kila mtu.

‘’Tunawaomba Watanzania wazidi kumuombea Rais wetu kasi aliyonayo aendelee kuwa nayo kwani Mungu anapenda haki katika maisha pamoja na uchumi ulio sawa’’

‘’Wakati mwingine hii kauli ya hapa kazi tu inakuwa hata sisi inatuogopesha lakini Mungu ataendelea kumlinda na kumwongoza,’’ amesema.

Naye Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assembles of God  TAG (CCC), Miyuji Dodoma, Samson Mkuyi amesema utawala wa Rais Magufuli umekuwa jibu la Watanzania wengi pamoja na kanisa.

Mchungaji Mkuyi amesema wanafurahishwa na utendaji kazi wake hasa kwenye upande wa maadili ikizingatiwa kuwa kanisa linataka maadili ya kiroho na kimwili.

‘’Tulianza kuyaomba haya miaka mitano sisi kama kanisa tunamwambia asiogope kwani Mungu yupo pamoja na yeye, sisi tunaendelea kumuombea ili mungu aendelee kumpa ulinzi,’’ amesema.

Wakati wa ibada hizo naye Askofu la Kanisa la Anglikana Central Tanganyika Dayosisi ya Kati, Dk. Dickson Chilongani aliwataka Watanzania kumuombea Rais Magufuli pamoja na Baraza lake la Mawaziri  ili waweze kuwafanyia kazi.

‘’Rais ameonekana kutumbua majipu yaliyokuwa yamejificha katika hili tutaendelea kumuombea ili aweze kuyayatumbua zaidi,pia na kuwafanya watendaji wafanye kazi kwa usahihi,’’ amesema.

Askofu Dk. Dickson Chilongani, amesema kuwa jukumu kubwa la linalofanywa na Rais Magufuli la utekelezaji wa kauli ya “hapa kazi tu, linapaswa kuombea na waumini na madhehebu ya dini zote ili kumkinga na maadui kwani ameleta matumani kwa watanzania.

Askofu Chilongani ameongea katika ibada maalumu ya kuadhimisha miaka 2,000 ya kuzaliwa kiongozi wa waumini wa dini hiyo, Yesu Kristo, katika kanisa kuu la Roho Mtakatifu, mjini Dodoma.

Askofu Chilongani amesema, maadhimisho hayo ni ishara tosha ya kuhakikisha wanaunga jitihada za Rais wa awamu  ya tano, kwani imechochea matumani mapya kwa wananchi ambao walikuwa wamekata tamaa.

Alitaja baadhi ya mambo yaliyokuwa yamekatisha tamaa na kuota mizizi ni pamoja na kuchoshwa na uroho wa wachache wanaotafuna rasilimali za watanzania.

Jingine ni ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya tunu za wanyama, mambo aliyosema yalikuwa ni wimbo uliojenga migogoro na matatizo, na kwamba wakati umefika sasa yamepata ufumbuzi.

“Tuna sababu ya kumuweka Rais wetu mikononi mwa Mungu, kwani tumepata kwa imani na kwa nguvu za maombi, hivyo ni lazima tuendelee kumwombea ili kazi anayofanya inaumiza waroho na wenye ubinafsi,” amesema.

Akipongeza juhudi za kile alichosema za utumbuaji majipu kupitia kauli yake ya “hapa kazi tu”, kuwa wasio na mapenzi mema sasa wamejenga roho za chuki naye.

Roho hizo mbaya pia zinachochea uovu mwingine wa kutaka kumwangamiza kwa jicho baya, hivyo kupitia maombi Mungu atampa kinga na ushindi na kumudu kutumbua majipu yaliyojificha sehemu mbaya zaidi.

Akipongeza juhudi za kazi alizofanya tangu ameingia madarakani miezi miwili iliyopita hadi sasa Watanzania wameongeza amani na upendo na kuendelea kuwa nchi ya kisiwa cha mfano wa kuigwa duniani kote.

Alisema amani hiyo inaleta matumaini kwa nchi zenye mafarakano kama Israeli ambayo muda mwingi wametumia mtutu na nguvu badala ya maongezi.

Katika hatua nyingine amewataka wananchi kumuunga mkono Rais Magufuli kwani kwa moyo alionyesha kwa Watanzania umeendelea kuweka mshikamano miongoni mwao kwa kudumisha amani, umoja na mshikamano.

error: Content is protected !!