January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majimbo matatu pima yetu – NLD

Spread the love

CHAMA cha National League for Democracy (NLD) kilichomo katika ushirikiano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kimeridhika na mgao wa majimbo inayoyawania kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Katika mgao uliofanywa baada ya majadiliano ya muda mrefu yaliyokuwa na misuguano, NLD kimepata majimbo matatu ya Lulindi, Masasi na Ndanda, yote yakiweko mkoani Mtwara, mkoa wa asili kwa Mwenyekiti Makaidi. 

Chama hicho kinachoongozwa na Dk. Emmanuel Makaidi, mwanasiasa mkongwe ambaye licha ya kukianzisha tangu mwaka 1992, na kushiriki uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi Oktoba 1995, hakijapata hata kimoja ndani ya ubunge, kilichukua uamuzi mgumu wa kuungana na Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kugomea Bunge Maalum la Katiba kikiwa na wajumbe wachache mno akiwemo yeye daktari.

Kaimu Katibu Mkuu wa NLD, Masudi Makujunga amesema kwamba wakati vyama vinavyounda UKAWA vikipata viti vingi vya kugombea, chama chao hakina cha kulalamika kwa sababu hata hayo ni “maendeleo makubwa kwetu katika kukijenga chama chetu.”

“Tumeangalia upeo wa kutafuta ushindi. Mtandao wetu haujaenea sehemu kubwa nchini. Tukatazama maeneo ambayo sisi tuna uwezo wa kukabiliana na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tukapata majimbo matatu.

“Maana yake ni kwamba sisi tumebaki katika sehemu tunayokubalika zaidi, kwani lengo letu ni kushinda na si ufahari kwamba sisi tumepata majimbo 10 ya kugombea wakati mtandao wetu haufiki mahala pengine,” amesema.

Makujunga amesema kutokana na ukiritimba wa serikali iliyopo madarakani, ya CCM, wanafanya shughuli za siasa kwa hali ngumu, wakikosa raslimali fedha na watu.

“Hatuna mtaji wa kutosha kuenea sehemu zote ndio maana tunafurahi kupata majimbo matatu ya Lulindi, Masasi na Ndanda ambayo tunayajua vizuri na tumewekeza kiasi fulani,” amesema huku akiwasihi wanachama na wafuasi wao kwenye maeneo mengine ya nchi, kushiriki kikamilifu kampeni zitakapoanza na kuunga mkono wagombea waliosimamishwa na vyama shirika na NLD vya UKAWA.

“Sisi kuwa na majimbo matatu haimaanishi tuna udhaifu. Hapana. Ndiyo tunayoyamudu. Hivyo, tunawaomba wanachama wetu nchini nzima wawapigie kura wagombea wa CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi ili kuiondoa CCM madarakani,” amesema.

Katika mgawanyo wa majimbo 253 kuwania ubunge, Chadema imeongoza kwa kupata majimbo 138, ikifuatiwa na CUF majimbo 99 (asilimia 29) yakiwemo 49 ya Zanzibar) na NCCR-Mageuzi majimbo 14 (asilimia 5.5).

error: Content is protected !!