May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majeruhi tukio la mauaji Dar wafanyiwa upasuaji Muhimbili

Hospitali ya Muhimbili kitengo cha Mifupa (MOI)

Spread the love

 

ASKARI Polisi wawili kati ya watano, waliojeruhiwa katika tukio la mauaji ya watu wanne, lililotokea karibu na Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania, wamefanyiwa upasuaji wa haraka, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi, tarehe 26 Agosti 2021 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma cha hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha, akizungumzia hali ya majeruhi hao waliowahishwa hospitalini hapo jana Jumatano.

Aligaesha amesema, majeruhi hao walifanyiwa upasuaji baada ya kuwa na majereha makubwa, na kwamba kwa zoezi hilo lilifanyika vizuri.

“Hospitali ya Taifa Muhimbili ilipokea majeruhi watano jana tarehe 25 Agosti, 2021, kuanzia muda wa saa saba mchana, wakiwa na majeraha makubwa na wengine madogo sehemu mbalimbali za miili yao. Ambapo wanne kati yao ni Askari wa Jeshi la Polisi na mmoja ni Mlinzi wa kampuni binafsi ya SGA,” imesema taarifa ya Aligaesha.

Taarifa hiyo imesema “mara tu baada ya kupokelewa, askari wawili ( miaka 41 & miaka 49) walikua na majeraha makubwa katika sehemu mbalimbali za Mwili na ya viungo vya ndani hivyo kufanyiwa upasuaji wa haraka ambapo upasuaji ulienda vizuri.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Askari wa tatu (miaka 35) aliyepata majeraha makubwa na madogo katika maeneo ya mikono na mgongoni, alipewa huduma za matibabu ikiwemo kufungwa vidonda.

“Askari wa nne (miaka 46), alitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani kwa kuwa alikua na majeraha madogo. Mlinzi wa SGA (miaka 42) naye alikuwa na majeraha ambayo hayakuhitaji upasuaji hata hivyo alilazwa wodini jana na ameruhusiwa leo kwenda nyumbani kuendelea na matibabu akiwa nyumbani,,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa ya Aligaeshi imesema, kwa sasa hospitali hiyo imebaki na majeruhi watatu, ambao wanaendelea na matibabu.

“Hivyo, tumebakiwa na majeruhi watatu ambao wanaendelea kupata matibabu na hali zao zinaendelea kuimarika. Hata hivyo, tulipokea mwili wa marehemu mmoja kutoka kwenye tukio hilo ambaye alikuwa ni mlinzi wa SGA na mwili wake umehifadhiwa chumba cha kuhifadhi maiti,” imesema taarifa hiyo.

Tukio hilo la mauaji lilifanywa na mtu aliyefahamika kwa jina la Hamza Mohammed, ambaye pia aliuawa wakati akijibizana kwa risasi na Askari Polisi.

error: Content is protected !!