July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majaribio ya dawa ya Ebola yaendelea Liberia

Spread the love

WATAALAMU wa tiba wameanza rasmi majaribio ya matumizi ya dawa ya kutibu ugonjwa wa ebola kwenye vituo vya afya vya mjini Monrovia.

Lengo la majaribio hayo ni kubaini kama dawa hiyo iliyotumika pia kutibu virusi vya magonjwa mengine inaweza kusaidia watu waliokumbwa na virusi hivyo.

Majaribio hayo ya dawa iliyopewa jina la ‘Brincidofovir’ yanasimamiwa na madaktari wa kundi la madaktari wasio na mipaka – Medicine Sans Frontiere (MSD). Dawa hiyo inaelezwa kuwa na uwezo wa kutibu aina mbalimbali za virusi, vikiwamo vile vinavyoshambulia wagonjwa waliofanyiwa tiba ya upandikizaji wa uboho (Bone Marrow Transplants).

Wakati majaribio hayo yakianza, mpaka sasa wataalamu hawajafanikiwa kupata uthibitisho hasa wa kupatikana dawa ya kutibu ebola, ugonjwa ulioleta maafa makubwa zaidi kwa kusababisha vifo vya watu 8,153 eneo la Afrika Magharibi.

Mbali na Liberia, ugonjwa huo umezikumba nchi za Siera Leone na Guinea. Liberia peke yake imepoteza watu 3,471 ikifuatiwa na Sierra Leone.

“Ni lazima ifahamike kuwa dawa hii si miujiza ya tiba, na haifahamiki kuwa itaweza kusaidia wagonjwa kuweza kupona,” imesema taarifa ya taasisi hiyo inayopigania afya njema kwa binadamu kote duniani.

Wagonjwa wapya watakaogundulika kuwa na ebola watajulishwa juu ya majaribio hayo na ni juu yao kuamua kufanyiwa majaribio au la.

Dawa hiyo si dawa pekee inayofikiriwa kutibu ugonjwa huo, dawa nyingine ni ZMapp ambayo majaribio yake yalifanywa kwa kutumia tumbili (nyani) 18 walioambukizwa virusi vya ebola.

Majaribio ya dozi ya ZMapp yaliwahi kutolewa kwa watu walioathirika na ebola. Hata hivyo, haijafahamiki vizuri kama dawa hiyo ndiyo hasa iliyofanikisha kuwatibu wagonjwa hao.

Dawa nyingine ni TKM-Ebola ambayo ni ya sindano na imetengenezwa na kampuni ya madawa ya Tekmira ya nchini Canada. Dawa hii inafanya kazi kwa kuzuia vinasaba vya ebola vinavyosaidia kuzaliana na kusambaa.

Majaribio zaidi

Jumanne wiki hii, kampuni kubwa ya madawa ya Marekani iitwayo Johnson & Johnson ilisema imeanza kufanya majaribio ya chanjo ya ebola kwa binaadamu.

Hatua ya kwanza ya chanjo hiyo inafanywa na kundi la watabibu wajuzi wa sindano kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, nchini Uingereza.

Majaribio hayo yanahusisha watu 72 ambao hawakuwa wameambukizwa virusi vya ebola, ambao waliamua kujitolea. Majaribio yataangalia ni jinsi gani miili yao inaweza kuhimili chanjo hiyo.

Kampuni hiyo imeahidi kutengeneza chanjo milioni 5 ndani ya miezi 12 mpaka 18 iwapo matokeo ya majaribio yatazaa matunda.

Takwimu za WHO

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), lililotoa taarifa yake mapema wiki hii, zaidi ya watu 20,000 wameambukizwa virusi vya ebola Afrika Magharibi hasa nchi hizo tatu za Liberia, Sierra Leone na Guinea tangu janga hilo lilipoanza.

Kuna zaidi ya waathirika 20,081 katika nchi hizo na zaidi ya vifo 7,842 vinavyohusishwa na ugonjwa huo.

Ebola inaendelea kusambaa kwa kasi Sierra Leone ambako taarifa ya WHO imesema kuna wagonjwa wapya 315 walioripotiwa kufikia wiki iliyoishia tarehe 21 Disemba, idadi ambayo inajumuisha wagonjwa 115 waliotokea mji mkuu wa Freetown.

Nchini Guinea, wagonjwa 156 waligunduliwa kwenye kipindi hichohicho, ikiwa ni kiwango kikubwa kutokea katika muda wa wiki moja tangu mlipuko huo uanze.

Kwa Liberia, kiwango cha maambukizi kimepungua kwa mwezi sasa na wiki iliyoishia tarehe 21 Disemba, kulikuwa kumegundulika wagonjwa 21 wapya.

Nchi nyingine tano za Nigeria, Senegal, Mali, Hispania na Marekani zimepata wagonjwa walioingia kutoka Afrika Magharibi na idadi yao imejumuishwa kwenye idadi ya jumla ya watu waliopata ebola.

Mgonjwa wa Uingereza

Pauline Cafferkey, mfanyakazi wa afya aliyekuwa nchini Sierra Leone na kuondoka tarehe 28 Disemba 2014, amegundulika kuwa na ebola. Mgonjwa huyo aligunduliwa na madaktari nchini Scotland, akiwa ndiye mgonjwa wa kwanza kupatikana nchini Uingereza.

Waziri Mkuu wa Scotland, Nicola Sturgeon alithibitisha kuwepo mgonjwa huyo ambaye ni mfanyakazi wa afya aliyekuwa mstari wa mbele kusaidia wagonjwa wa ebola waliokuwa kwenye kambi za kutibu wagonjwa wengine.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Nicola amesema kwa sasa anaendelea vizuri. Shirika la Save the Children lilithibitisha kuwa mfanyakazi huyo ni mwajiriwa wa Wizara ya Afya ya Uingereza (NHS) anayefanya kazi na shirika hilo.

Mpaka tarehe 21 Disemba, wafanyakazi 666 walikuwa wamegundulika kuambukizwa ebola; kati yao, 366 wakiwa wamepoteza maisha, kwa mujibu wa WHO.

Mlipuko wa ebola uliotokea mwaka mmoja kwa mgonjwa wa kwanza kupatikana nchini Guinea, huenda utaendelea mpaka mwishoni mwa mwaka huu wa 2015, kwa mujibu wa Mwanasayansi Peter  Piot ambaye alisaidia kugunduliwa kirusi hicho mwaka 1976.

Ingawa chanjo ya kutibu ebola haijapatikana, shirika la afya ulimwenguni limeruhusu matumizi ya dawa   zisizojaribiwa ili kudhibiti ugonjwa huo.

*Habari hii imeandikwa na Benedict Kimbache kutoka vyanzo mbalimbali.

error: Content is protected !!