July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majangili kuwindwa kwa silaha za kivita

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akikagua askari wa wanyamapori alipotembelea chuo cha wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza

Spread the love

WANAFUNZI wanaosomea uhifadhi wa wanyamapori, kwa sasa wataanza kujifunza kutumia silaha za kivita ili kukabiliana na ujangili kwa kutumia vifaa vya kisasa zaidi. Anaandika Mwandishi wetu, Mwanza (endelea).

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amesema hayo jana alipotembelea chuo cha wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza kwamba, ili kukabiliana na majangili ambao wanatumia silaha nzito, tayari serikali imeingiza nchini bunduki za rashasha AK 47 ili askari hao waweze kukabiliana na majangili.

“Nataka niwahahakikishie kuwa kila askari atakuwa na darubini (miwani) ya kuona kwenye giza na fulana ya kuzuia risasi ili tusipoteze askari wetu kwa majangili,” amesema.

Amesema vifaa hivyo vimeanza kuwasili na vingine vingi vitakuja kwani kwa sasa mafunzo ya kijeshi yameanza kwa askari walioporini kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi Tanzania, Polisi na Jeshi la Marekani Komandi ya Afrika, ambapo askari wote watapewa mafunzo hayo.

Nyalandu amesema utaratibu unaotumika kwa sasa unaleta usumbufu kwani urasimu unasababisha askari hao wanapomaliza mafunzo kusubiri kusailiwa wakati wa ajira wakati kuna upungufu mkubwa wa askari hao.

“Hatuwezi kukaa na kusubiri kupata kibali cha sekretarieti ya ajira kwa maana sasa hivi tumeanzisha Mamlaka ya Wanayamapori na kwa hiyo watakuwa na uwezo wa kuajiri moja kwa moja kuliko utaratibu wa sasa unaofanya mwanafunzi akimaliza chuo asubiri kusailiwa; mbona polisi na jeshi hawafanyi hivyo? Amehoji.

Waziri Nyalandu ameongeza kuwa, kwa sasa kuna tatizo kubwa la ujangili na kuahidi kuwa vijana wengi watakaopata mafunzo wataajiriwa ili vita ya kupambana na majangili nchini ielekezwe sehemu zote ili kuweza kulinda na kuhifadhi rasilimali nchini kwa ajili ya vizazi vijavyo.

“Tumefanikiwa Serengeti na Selous lakini kwa sasa janga kubwa limekuwa katika pori la Rungwa ambalo limeungana na Ruaha, tembo wengi wamekuwa wakiuawa na sasa vita tunaelekeza huko, ili kumaliza tatizo la ujangili,” amesema.

Nyalandu ambaye alitembelea chuo hicho kukagua maendeleo ya mradi wa maboresho ya chuo unaofadhiliwa na Howard Buffet Foundation (HGBF) kwa kupitia taasisi yake ya uhifadhi ya Nature Conservation Trust, aliagiza ujenzi wa bweni la wanafunzi 300 ukamilike katika kipindi kifupi kwa kuwa fedha za mradi zipo tayari.

Mkuu wa chuo hicho, Lowaeli Damalu alimshukuru Nyalandu kwa kutafuta mfadhili huyo na kusema kuwa kwa sasa chuo kimekuwa cha kisasa na vifaa vya kutosha kwa kufundishia.

Alisema kwamba msaada huo unaokaribia Sh. 4 bilioni umewezesha kununua vitabu, magari, mahema darubini na kompyuta maalum ambavyo unaweza kuwajenga wanafunzi kufanya kazi watakapoajiriwa kwa weledi mkubwa.

Dumalu alisema kwamba kwa sasa bwalo la chakula limekamilika na fedha kwa ajili ya ujenzi wa bweni ziko tayari lakini tatizo limekuwa ni kwa mkandarasi, ambaye aliweka bei kubwa kupita bajeti na hivyo kumwahidi waziri kuwa mkandarasi ataletwa na mfadhili ili kukamilisha mradi huo kabla ya mwisho wa mwaka.

Mbali na kuboresha mafunzo kwa wanafunzi lakini pia walimu wamepata fedha kutoka HGBF kwa ajili ya mafunzo kwa walimu na wafanyakazi ambao wamekuwa wakiendelea na mafunzo hayo kazini ili kuweza kupambana na ujangili na kwamba mradi huo bado unaendelea.

error: Content is protected !!