May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa: Simba wameupiga mwingi

Spread the love

 

WAZIRI mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Kassim Majaliwa, ameipongeza klabu ya soka ya Simba kwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa mara baada ya kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la Shirikisho Barani Afrika. Anaripoti Kelvin Mwaipungu…(endelea)

Majaliwa ameyasema hayo hii leo Bungeni jijini Dodoma, wakati akisoma hotuba yake kuhusu mapitio na mwelekeo wa Serikari na makadilio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2022/2023.

Katika hotuba yake Waziri Mkuu alitumia nafasi hiyo ya kipekee kuipongeza klabu hiyo ambayo kwa sasa ipo hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu ndani ya bara la Afrka.

“Kipekee niipongeze timu ya Simba Sports Club kwa kupeperusha bendera ya Taifa letu katika mashindano ya Shirikisho la Klabu Afrika. Mwenye macho haambiwi tazama, sote tumeshuhudia wakiendelea kuupiga mwingi na kutuwakilisha vema katika medani za kimataifa.” Alisema Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa

Katika michuano hiyo, tayari klabu ya Simba imepangwa kucheza na Orlando pirates kwenye hatua hiyo ya robo fainali mara baada ya kuchezeshwa kwa droo siku ya jana  tarehe 5 Aprili 2022.

Mchezo huo wa kwanza wa michuano hiyo utapigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na mchezo wa pili utapigwa Soweto nchini Afrika Kusini tarehe 24 Aprili 2022.

Aidha Waziri Mkuu hakusita kuzipongeza klabu zingine zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi Kuu Zanzibar kwa kuendelea kusisitiza umuhimu wa michezo nchini.

error: Content is protected !!