May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa: Si sera ya Serikali kuwaonea waandishi wa habari

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema, sio sera ya Serikali kuwaonea waandishi wa habari wanaotekeleza majukumu yao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro…(endelea).

Majaliwa amesema hayo leo Alhamisi, tarehe 20 Mei 2021, katika mkutano wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), uliofanyika mkoani Morogoro.

Ametoa kauli hiyo, baada ya jukwaa hilo kuwasilisha kwake malalamiko ya baadhi ya waandishi wa habari, kushambuliwa na maafisa wa Serikali wakitekeleza majukumu yao.

Majaliwa amesema, Serikali haitavumilia mtu yeyote atakayemkwaza mwandishi wa habari wakati wa utekelezaji majukumu yake.

“Wala sio sera ya serikali kuonena waandishi wa habari, serikali haitavumilia mtu yeyote atakayemkwaza mwandishi wa habari akiwa katika kazi ya uandishi wa habari na niwahakikishie kuwa, hatua kali itachukuliwa dhidi yake,” amesema Majaliwa.

Waziri mkuu huyo amesema, Serikali itaendelea kulinda misingi ya habari huku akiwataka wadau wa tasnia hiyo kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.

“Serikali itaendelea kuimarisha misingi ya habari tuliyo nayo nchini, kwa upande wenu zingatieni sheria za nchi, msitumie vibaya kalamu zenu. Ni muhimu sana kalamu yenu itumike kusimamia haki ya kila mmoja,” amesema Waziri Majaliwa.

Tarehe 21 Aprili 2021, Mwandishi wa Habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Jesse Mikofu, alishambuliwa na baadhi ya askari wa Vikosi vya Jeshi la Polisi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), akitekeleza majukumu yake.

Mwandishi huyo alikumbwa na mkasa huo, baada ya kuwapiga picha askari hao waliokuwa wanatekeleza jukumu la kuwahamisha wamachinga waliopanga bidhaa zao barabarani.

error: Content is protected !!