May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa: Dk. Magufuli ameacha alama hadi vijijini

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema, aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli, alikuwa kiongozi mahiri na ameacha alama Taifa zima na ndiyo sababu analiliwa na wananchi nchi nzima hadi vijijini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Ameyasema hayo leo Jumatano, tarehe 24 Machi 2021, alipozungumza na wananchi kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kabla ya shughuli za kuaga mwili wa Hayati Magufuli ambayo iliongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.

“…mpendwa wetu kaka yetu kiongozi wetu Dk. John Pombe Magufuli alikuwa kiongozi shupavu, aliyeliongoza Taifa hili kwa umahiri mkubwa na Mwanza ni mahali pa kihistoria kwa kiongozi wetu, ameishi hapa, amefanya kazi hapa na katika utumishi wake amefanya mambo makubwa ambayo yameweka alama kwenye mikoa hii ya Kanda ya Ziwa,” amesema.

Akiwasilisha salamu za Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema Rais anawapa pole wanakanda ya ziwa na anawasihi katika kipindi hiki cha majonzi wawe watulivu, waendelee kushikamana, kushirikiana na kupendana kama ilivyokuwa awali.

Amesema kila mwananchi kwa dini yake na dhehebu lake aendelee kumuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Hayati Magufuli pahala pema.

Majaliwa amesema, baada ya viongozi kumaliza kuaga uwanjani hapo, mwili umezungushwa katika uwanja huo mara tano ili kutoa nafasi kwa wananchi kumuaga Hayati Magufuli na kisha mwili umezungushwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza na baadaye safari ya kwenda nyumbani kwao Chato, mkoani Geita kwa.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa baada ya mwili huo kuzungushwa katika jiji hilo, utaelekea Chato mkoani Geita kwa kupita katika daraja la Kigongo-Busisi na mwili utakapofika hapo utasimama kwa dakika kumi ili kutoa fursa kwa wakazi wa eneo hilo ambapo ni nyumbani kwa mke wa marehemu kuaga mwili wa hayati Dkt. Magufuli.

Mapema asubuhi, Majaliwa aliwaongoza viongozi mbalimbali na wananchi wa mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani kuupokea mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Magufuli katika uwanja wa ndege wa Mwanza.

Vilio, huzuni na simanzi zilitawala kwa wananchi waliojipanga pembezoni mwa barabara kuanzia uwanja wa ndege wa Mwanza hadi uwanja wa CCM Kirumba, ambapo ulipofika katika eneo la Nyamanoro ambako marehemu aliwahi kuishi msafara ulisimama ili kutoa fursa kwa waliokuwa majirani kumuaga.

Hayati Magufuli alifariki dunia Jumatano ya tarehe 17 Machi 2021, katika hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa Ijumaa 26 Machi 2021, wilayani Chato mkoani Geita.

error: Content is protected !!