Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Majaliwa awapa siku 30 Ma-RC kuwapanga machinga
Habari za Siasa

Majaliwa awapa siku 30 Ma-RC kuwapanga machinga

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewapa muda wa mwezi mmoja (siku 30) viongozi wa mikoa na halmashauri wawe wamekutana na wafanyabiashara wadogo maarufu wamachinga na kupanga namna bora ya usimamizi wa shughuli za biashara ikiwemo kutenga maeneo ya kufanyia biashara zao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa jana Jumanne, tarehe 14 Septemba 2021, wakati akizindua mpango wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi wa 2022, ambapo aliwataka Wakuu wa Mikoa wawe makini katika zoezi la kuwapanga Wamachinga nchini na kuepuka vurugu, fujo na uonevu.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano, wakati akizungumza kwa njia ya video na Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Waziri wa Viwanda na Biashara, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Uongozi wa Wamachinga.

Waziri Mkuu amewaelekeza viongozi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na wilaya waone namna ya kutumia baadhi ya barabara za katikati ya majiji na miji kufungwa muda wa alasiri ili kuruhusu Wamachinga kufanya biashara zao katika barabara hizo, “hii ni fursa nzuri kwa wajasiriamali wetu kufanya shughuli zao.”

Amesema viongozi hao wa mikoa kwa kushirikiana na viongozi wa machinga na machinga wanaweza kutenga maeneo maalumu na kuanzisha magulio ya mwishoni mwa wiki, utaratibu huo utawezesha wajasiriamali wengine kufanya shughuli zao za kiuchumi kama madereva wa bodaboda, machinga na taksi watakaokuwa wakisafirisha abiria.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wahakikishe maeneo watakayoyatenga kwa ajili ya wamachinga kufanya biashara zao yanatambulika na yanakuwa na miundombinu muhimu kama vyoo, maji ili kuyaboresha.

Majaliwa amesema Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara ina mkakati wa kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo kwa lengo la kuwapa uelewa mpana wa biashara wanazofanya.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ummy Mwalimu amesema wamepokea maelekezo hayo na kwamba tayari wameshaanza kuandaa muongozo wa kuratibu shughuli za Wamachinga ambao utawawezesha viongozi wa mikoa kuweza kuwasimamia wafanyabiashara hao.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo ametumia fursa hiyo kuwahakikishia Wamachinga pamoja na wafanyabiashara wadogo nchini kwamba kwa sasa rasmi Serikali katika sera ya Biashara Ndogo ndogo (SME) nchini imewatambua Wamachinga.

Awali, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga Tanzania, Ernest Matondo Masanja pamoja na mambo mengine ameishukuru Serikali kwa hatua inazochukua kuhusu Machinga na kwamba ameahidi kuendelea kushirikiana nayo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!