Tuesday , 23 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Majaliwa awahamasisha wananchi kujikita kwenye kilimo
Habari za Siasa

Majaliwa awahamasisha wananchi kujikita kwenye kilimo

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambaye pia ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua daraja la mto Sibiti, linalounganisha Mkoa wa Singida na Simiyu
Spread the love

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Singida waingie kwenye kilimo cha kisasa ili waweze kuinua uchumi wao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Singida … (endelea).

“Wananchi ingieni kwenye kilimo cha Kisasa na chenye tija ili muinue kipato chenu. Hili eneo la Gumanga ni zuri sasa kwa kilimo na wengi wenu wanalima mbogamboga.

“Vijana msikae kusubiri ajira za ofisini, ajira siyo lazima ukae ofisini, unaweza kujiajiri kwenye kilimo,” alisema.

Majaliwa ametoa kauli hiyo jana Jumanne tarehe 15  Septemba 2020 wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano wa kuwanadi mgombea ubunge wa Iramba Mashariki, Francis Mtinga na mgombea udiwani, James Mkwega uliofanyika viwanja vya stendi ya mabasi Gumanga, wilayani Mkalama, mkoani Singida.

Majaliwa ambaye alikuwa mkoani Singida kumuombea kura mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, John Pombe Magufuli, alisema Serikali inatekeleza kwa vitendo ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025 na moja ya mkakati wake ni kutoa fursa tofauti ili wananchi waweze kunufaika.

“Huku Singida ni wakulima wazuri wa alizeti na mna viwanda vingi vya kusindika mafuta. Tumieni fursa hii ya kilimo kuinua kipato chenu, Serikali yenu itaendelea kuboresha fursa za uwekezaji.”

Mapema, mgombea ubunge wa jimbo la Iramba Magharibi na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwigulu Nchemba aliwataka wakazi wa Singida wasifanye mzaha kwenye masuala ya uchumi.

“Tuache mzahamzaha katika masuala ya uchumi na maendeleo na siku ya tarehe 28 Oktoba, tufuatane wote tukapige kura kwa Dkt. John Pombe Magufuli. Raha ya ushindi ni kuwa na kura nyingi za Rais, Wabunge na madiwani,” alisema.

Naye mbunge aliyemaliza muda wake, Allan Kiula aliahidi kusaidiana na Mtinga kufanya kampeni ili kuhakikisha Chama cha Mapinduzi kinapata ushindi mkubwa.

“Tutasaidiana na Francis Isack kutafuta kura za CCM. Tutafanya hivyo pia kwa ajili ya kura za madiwani wetu. Tunahitaji madiwani wa kutosha ili Isack aweze kupata timu ya kufanya nayo kazi kwa urahisi,” alisema.

Katika hatua nyingine,  Majaliwa ameagiza ekari 2,500 kati ya ekari 5,432 zilizoko kwenye kijiji cha Sagala zirejeshwe kwa wananchi ili zitumike kwa kilimo.

“Tunaboresha uchumi ili ushuke kwa wananchi iwe kwenye kilimo, uvuvi au ufugaji. Nina taarifa kuwa Halmshauri ya Singida kwenye Kijiji cha Sagala wamechukua ekari 5,432 na kuamua kuzikodisha kwa wannchi wakidai kuwa ni kitega uchumi cha Halmashauri.”

“Wao hawalimi, na kama hawana cha kufanya kwenye eneo lile, walirudishe kwa wananchi. Mkuu wa Mkoa wa Singida, uende kule na uanze mchakato wa kupunguza eneo hilo ili yapatikane mashamba ya kuwagawia wananchi. Nasikia wanawakodisha kwa Sh.50,000.”

“Najua hawawezi kulima ekari zote 5,000. Nenda kawapunguzie ekari 2,500 ili wagawiwe wananchi. Ingekuwa mjini hapa Ilongero, tungesema wanataka kupima viwanja na ningewasamehe, lakini kule ni mbali lazima warudishe hilo eneo kwa wananchi,” alisema na kuamsha shangwe kwa wananchi hao.

Aliwataka wananchi hao watakapopatiwa eneo hilo, walime kwa bidii ili mazao yao yaweze kuuzwa mjini na kwenye kata ya Ilongero.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia aridhishwa utendaji mabalozi, awapa neno

Spread the loveRais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amewapongeza mabalozi  wanaowakilisha ...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mbunge ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the loveMBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze kasi...

error: Content is protected !!