Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Majaliwa atoa ujumbe kwa taasisi za dini
Habari Mchanganyiko

Majaliwa atoa ujumbe kwa taasisi za dini

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaheshimu, inathamini na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za kidini katika kujenga jamii ya wacha Mungu, wenye kutii mamlaka na sheria. Anaripoti Patricia Kighono,TUDARCo … (endelea).

Pia, Majaliwa ametoa wito kwa taasisi za kidini kujiepushe kutumia nyumba za ibada kama majukwaa ya siasa na badala yake ziendelee kushirikiana na Serikali katika kujenga Taifa la watu wenye hofu ya Mungu, heshima, upendo na wenye kudumisha amani na utulivu nchini.

Majaliwa ameyasema hayo leo Ijumaa, tarehe 1 Oktoba 2021, kwenye hafla ya uzinduzi wa msikiti wa Jamiu Assaliheen uliojengwa na taasisi ya Istiqaama katika Kata ya Ikwiriri, wilayani Rufiji, Pwani.

Msikiti huo una uwezo wa kutumiwa na waumini 500 kwa wakati mmoja na una vyumba vinne vya madrasa kwa ajili ya kutoa elimu ya dini na malezi mema.

Majaliwa amesema Serikali kwa upande wake itaendelea kushirikiana na taasisi zote za kidini zenye nia safi na thabiti ili kuhakikisha miradi na mipango mbalimbali ya kijamii na kiroho yenye manufaa kwa umma wa Watanzania inaendelea kutekelezwa kama ilivyokusudiwa.

“Sote ni mashahidi kuhusu mchango mkubwa unaotolewa na madhehebu au taasisi za kidini katika jamii yetu.”

Taasisi za kidini nchini zimekuwa zikijihusisha kwa kiwango kikubwa na utoaji wa huduma za kijamii hususan elimu, maji, afya, kusaidia watu wenye uhitaji kama vile yatima na wajane sambamba na malezi na utoaji wa huduma za kiroho.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Jumuiya ya Istiqaama kwa kazi nzuri wanazozifanya nchini ikiwemo ya kujenga mshikamano baina ya waislamu wa madhehebu mbalimbali lakini pia baina ya waislamu na waumini wa dini nyingine.

“Hivyo basi, tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atujaalie sote moyo wa subra na kujitolea katika mambo ya heri,” amesema Majaliwa

“Aidha niwapongeze kwa kazi nzuri ya kujenga misingi mizuri ya kiroho na kimaadili kwa vijana wetu ambao ndiyo Taifa na viongozi wetu wa kesho. Jambo hili ni la msingi sana kwani ni dhahiri kuwa hakuna Taifa lolote duniani linaloweza kufanikiwa bila ya kuwa na misingi imara ya kiroho na kimaadili.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Jumuiya ya Istiqaama Tanzania, Sheikh Badar bin Sood amempongeza Rais Samia kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuendeleza umoja, amani, mshikamano na maendeleo kwenye kila nyanja kwa Watanzania wote.

Naye, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar bin Zubeir bin Ally amewakumbusha waumini wa dini ya kiislam na watanzania kwa ujumla kujitokeza kuchanja chanjo ya ugonjwa wa UVIKO 19 ili kuongeza kinga na kujilinda na ugonjwa huo.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Mkuu wa Jumuiya ya Istiqaama Tanzania Sheikh Khalifa, Sheikh, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Istiqaama Tanzania, Sheikh Seif Ally Seif, Naibu Balozi wa Oman nchini, Dkt. Salim Al Harbin, Mwakilishi wa Mufti wa Oman, Sheikh Dr Wail Al Harasi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Puma Energy Tz: Watanzania tudumishe amani kuvutia uwekezaji

Spread the loveKAMPUNI ya Mafuta ya Puma Tanzania imewakutanisha wadau mbalimbali katika...

Habari Mchanganyiko

DAWASA waanza utekelezaji agizo la Samia

Spread the loveMamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam...

Habari MchanganyikoKimataifa

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the loveTUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais wa...

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

error: Content is protected !!