May 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa atoa siku 15 hospitali ya Uhuru ikamilike

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua jengo la Hospitali ya Uhuru inayojengwa na Serikali katika wilaya Chamwino, Dodoma

Spread the love

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ametoa siku 15 kwa uongozi ya Wilaya ya Chamwino, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Suma JKT wahakikishe ujenzi wa hospitali ya Uhuru Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma unakamilika. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo, leo Ijumaa tarehe 20 Novemba 2020, Majaliwa amesema, lengo ni kuhakikisha hospitali hiyo inazinduliwa na Rais John Pombe Magufuli ifikapo 9 Desemba 2020 ili kutimiza maono yake ya ujenzi wa hospitali hiyo.

“Nimeridhika na hatua hii ya ujenzi lakini haitoshi, hamieni hapa, huu ni wakati wa kazi, hakikikisheni kazi inafanyika usiku na mchana ili 5 Desemba 2020 kazi ikamilike na 9 Desemba 2020 izinduliwe,” amesema Majaliwa

Aidha, Majaliwa amesema,anataka kuona vifaa vyote vya ujenzi wa hospitali hiyo vinatoka kwenye viwanda vya ndani ili kuharakisha ukamilishwaji wa hospitali hiyo hasa marumaru kwani tayari tuna viwanda vikubwa vinavyozalisha bidhaa hiyo kwa ubora wa hali ya juu.

“Mnabishana kuhusu uwekaji wa tiles, mnataka za nje? TBA mnang’ang’ania kununua tiles kutoka nje ya nchi, kwa nini? Sisi tumehamasisha ujenzi wa viwanda na viwanda vipo vinavyotengeneza tiles tena nzuri, tuna kiwanda Chalinze kikubwa sana na kingine kipo Mkuranga, hata jengo letu la Tume ya Taifa ya Uchaguzi tumeweka tiles za ndani, na bora mshitiri hujazinunua, na usinunue kutoka nje, tuna viwanda vipo nchini,” amesisitiza.

Jengo la Hospitali ya Uhuru inayojengwa na Serikali katika wilaya Chamwino, Dodoma

Akitoa taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (TAMSEMI), Mhandisi Joseph Nyamhaga amesema, ujenzi wa hospitali hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli alilolitoa kuwa kiasi cha Sh.995.1 milioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 57 ya Uhuru mwaka 2018 zitumike katika ujenzi wa hospitali hiyo.

Pia, Januari 2019, wakati akipokea gawio la hisa za kampuni ya simu ya Airtel, aliagiza kiasi cha Sh. 2.415 bilioni zitumike kwenye ujenzi huo.

Akielezea mipango ya baadaye, Mhandisi Nyamhanga amesema kwa mwaka 2020/2021, Serikali imepanga kuendelea na ujenzi wa hospitali za halmashauri 27 ambazo kila moja imetengewa Sh.1 bilioni.

Aidha, alisema Sh.27.75 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati 555 ambapo zahanati tatu zitajengwa kwa kila Halmashauri na kila zahanati inagharimu Sh.50 milioni.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Kanali Laurence Lukema amesema wao kama wakandarasi wa ujenzi, watahakikisha ujenzi wa hospitali hiyo unakamilika kwa wakati.

error: Content is protected !!