WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameliagiza Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), liongeze juhudi katika usimamizi wa taasisi na vyuo vya elimu, ili vitoe elimu bora yenye kukidhi matakwa ya soko la ajira duniani. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).
Waziri Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Ijumaa, tarehe 28 Mei 2021, akifungua maonesho ya pili ya elimu na mafunzo ya ufundi, katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
“Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, imeweka wazi kuwa elimu ni kipaumbele cha juu. Kwani ndiyo kitovu cha kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwenye jamii. Vyuo na taasisi zinazotoa elimu hii, ni lazima vihakikishe vinatoa elimu bora inayokidhi viwango na mahitaji ya soko la sasa la ajira” amsema Waziri Majaliwa.
Aidha, Waziri Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuweka sera zinazotoa fursa kwa wadau mbalimbali, kuwekeza katika sekta ya elimu na hivyo, kuunga mkono juhudi za kuliletea Taifa maendeleo.

“Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za umma na binafsi ambazo zinatoa elimu na mafunzo ya ufundi hapa nchini. Hivyo, natoa wito kwa wadau wote kuungana na Serikali kuwekeza katika utoaji wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika fani mbalimbali,” amesema Waziri Majaliwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, amesema wizara hiyo itaendelea kuhakikisha inatoa elimu ya mafunzo ya ufundi stadi, kwa kuzigatia mahitaji ya soko ya kipindi husika na kuwaandaa vijana kwa siku zijazo.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uongozi NACTE, Prof. John Kondoro, amesema watashirikiana na vyuo, taasisi za elimu ya mafunzo ya ufundi na wadau wengine, kusimamia utoaji wa mafunzo ili kuhakikisha elimu ya ufundi na mafunzo, inatolewa kwa ubora ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira la ndani na nje.
Leave a comment