September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa atoa maagizo mazito TARURA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wahandisi wa Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) kusimamia miradi kwa weledi, uadilifu na uaminifu huku wakizingatia ubunifu kwa kutumia teknolojia mpya, sahihi na rafiki kulingana na upatikanaji wa malighafi za ujenzi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Pia ameiagiza TARURA kufanyia kazi haraka, maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kujifunza teknolojia inayotumiwa kutengeneza barabara za Zanzibar ambayo imeonesha kuwa nafuu na ya viwango vya juu.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo tarehe 12 Februari, 2022 alipofungua Mkutano wa Kazi kati ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, TARURA, Wakandarasi, Bodi ya Usajili wa Wakandarasi, Mfuko wa Barabara na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma jijini Dodoma.

Amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali katika kuijengea uwezo TARURA ili kutekeleza makujumu yake ikiwa ni pamoja kuiongezea fedha kutoka sh. bilioni 247.5 ilipoanzishwa mwaka 2017 hadi kufikia Sh. bilioni 752.61 sawa na ongezeko la asilimia 204.3.

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Kazi kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, TARURA na Wakandarasi, wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati alipofungua mkutano huo, uliofanyika katika ukumbi wa St. Gasper Jijini Dodoma, Februari 12, 2022.

“Fedha hizo zinajumuisha sh. bilioni 127.50 kutoka Serikali Kuu, sh. bilioni 272.50 kutoka Mfuko wa Barabara, sh. bilioni 322.15 kutoka katika tozo ya sh. 100 kwa lita ya mafuta ya petroli na dizeli na sh. bilioni 30.44 kutoka kwenye ushuru wa maegesho wa magari,” amesema.

Amesema mwaka 2017, TARURA ilikuwa inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 108,946.19 na sasa mtandao huo umeongezeka na kufikia kilomita 144,429.77 ambazo zimetangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali Na. 463 la tarehe 25 Juni 2021.

Majaliwa ameongeza kuwa wakati TARURA inaanzishwa mwaka 2017, barabara za lami zilikuwa kilomita 1,449.55 sawa na asilimia 1.30 na sasa ni kilomita 2,473.55 sawa na ongezeko la kilomita 1,024 sawa na asilimia 70.6.

Pia ameiagiza Ofisi ya Rais-TAMISEMI ifuatilie na kuchukua hatua stahiki kwa Halmashauri zote zitakazoshindwa kutekeleza kazi za matengenezo ya barabara kulingana na mkataba wa makubaliano.

“Usimamizi wa taratibu za utoaji wa zabuni ufanyike kwa umakini na kwa kuzingatia sheria. Mikataba ya kazi isainiwe kwa wakati, pia tathmini za zabuni zizingatie Sheria ya Ununuzi wa Umma na zihusishe upekuzi ili kupata makandarasi wenye uwezo na kukidhi vigezo stahiki,” amesema.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza TARURA kuaza kutekeleza mpango wa uwekaji taa za barabarani wakati wa ujenzi wa barabara.

“Hakikisheni hii inakuwa sehemu ya mkataba wa ujenzi wa barabara zote zinazojengwa, jifunzeni utaratibu huu kutoka TANROADS ambao tayari wanautekeleza” amesema.

Waziri Mkuu amewataka wakandarasi wazawa wajiimarishe katika kazi zao za ujenzi wa barabara ili waweze kufanya kazi yenye ubora, kwa wakati na viwango.

Amewaagiza watumishi wa TARURA wasijiingize kwenye kazi zenye mgongano wa maslahi.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff awasilishe kwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi orodha ya wakandarasi wababaishaji na awasilishe nakala kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI ili iwasilishwe kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kwa hatua zaidi za kinidhamu.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa amesema Serikali ina matumaini makubwa kupitia watendaji hao na kwamba changamoto zote zinazowakabili hazina budi kufanyiwa kazi kwa wakati ili waweze kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Waziri Bashungwa ameagiza asilimia 60 ya kazi za TARURA zitangazwe mapema, bila kusubiri mpaka mwaka wa fedha uanze ili pale mwaka wa fedha unapoanza iwe ni wakandarasi kuanza kazi.

Awali, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Seff amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni pamoja na baadhi ya makandarasi kuomba kazi nyingi na wakati mwingine kupata kazi nyingi kuliko uwezo wao.

“Hivyo tulazimika kusubiri hadi kazi iishe eneo fulani ndipo wapeleke vifaa na ku4anza kazi eneo jingine,” amesema.

error: Content is protected !!