Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Majaliwa atoa maagizo kwa mawaziri, azuia walinzi binafsi
Habari za Siasa

Majaliwa atoa maagizo kwa mawaziri, azuia walinzi binafsi

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa
Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaagiza mawaziri na naibu waziri wasimamie taasisi na idara zilizopo chini ya wizara zao ili zizingatie vigezo vyote vya utawala bora pamoja na kukomesha vitendo vya rushwa ambavyo ndio adui mkubwa wa utawala bora. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

“Ninapenda kuwakumbusha kuwa ninyi ni nyenzo muhimu katika utendaji wa Serikali, hivyo wazembe, wezi na wabadhirifu waliopo chini ya mamlaka zenu lazima wote wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Serikali. Kila kiongozi lazima awe makini muda wote.”

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Ijumaa, tarehe 29 Oktoba 2021, wakati alipofungua Mafunzo ya Uongozi kwa Mawaziri na Naibu Mawaziri katika Ukumbi wa Mtakatifu Gasper jijini Dodoma. Mafunzo hayo yameandaliwa na Taasisi ya Uongozi.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kupanua uelewa wa mawaziri na naibu mawaziri kuhusu masuala mbalimbali ya uongozi ikiwa ni pamoja na kuelewa majukumu, madaraka na mipaka ya nafasi zao, kuongoza watu, kufanya maamuzi ya kimkakati na kuboresha sifa binafsi za kiuongozi.

Amesema ubadhirifu unatakiwa ushughulikiwe mapema kwa weledi na utaalam bila kulazimika kusimamisha utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa muda mrefu na hatua zichukuliwe bila kuoneana haya kama kuna ushahidi wa wazi kabla hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hajakagua au viongozi wa juu kuchukua hatua.

Amewataka viongozi hao kutumia mada zitakazowasilishwa ili ziweze kuwasaidia katika kuzisimamia vyema Wizara wanazoziongoza na taasisi zilizo chini ya wizara zao “mwende mkazisaidie taasisi hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yake bila kikwazo chochote. Nendeni mkawe msaada kwao.”

Kadhalika, Majaliwa amewataka viongozi hao kwa kushirikiana na Taasisi zingine waendelee kusimamia amani na utulivu kwenye maeneo yao ili watu waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote.

“Amani na utulivu ndiyo itatuwezesha kama nchi, tuendelee kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza mitaji yao hapa nchini.”

“Tunakumbushwa sisi viongozi wa Tanzania tuwe wazalendo na tuhakikishe tunaziendeleza rasilimali za nchi hii kwa faida ya Watanzania wote bila ubaguzi wa jinsia, kabila, dini na rangi ili mradi mtu hajavunja sheria. Tuwahudumie Watanzania wote kwa usawa.”

Pia, Majaliwa amewasisitiza viongozi hao waepuke matumizi ya walinzi binafsi na waandishi wa habari binafsi katika Ofisi za Umma kwani wanaweza kuwa chanzo cha uvujaji wa siri za Serikali.

“Upo utaratibu wa kufuata endapo itabainika mnahitajika kupatiwa wasaidizi hao. Zingatieni utaratibu huo na si vinginevyo.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Managementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa ameiagiza Taasisi ya Uongozi ihakikishe inaendelea kuandaa mafunzo ili kujadili masuala mbalimbali kuhusu miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini, hususan ile inayosimamiwa na Ofisi ya Rais.

“Nia ni kutoa ujuzi, maarifa na taarifa kwa viongozi kutoka kwenye sekta mbalimbali juu ya umuhimu wa miradi hii. Kutokana na umuhimu wa miradi ya kimkakati, mikutano hii ni ya lazima.”

Pia, Waziri Mchengerwa ameziagiza wizara, idara na taasisi zote za Serikali zihakikishe zinatenga bajeti kwa ajili ya kuwapeleka watumishi viongozi kushiriki katika mafunzo yanayoandaliwa na kutolewa na Taasisi ya Uongozi ili kuwaimasha kiutendaji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!