May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa ateta na Rais wa CAF

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Dk. Patrice Motsepe ofisi kwake Mlimwa jijini Dodoma na kujadiliana kukuza soka nchini. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Wawili hao walikutana leo Ijumaa Agosti 13, mwaka huu na ndio mara ya kwanza tangu achaguliwe kuchukua nafasi hiyo kwenye mkutano Mkuu wa shirikisho hilo uliofanyika Machi 12, mwaka huu.

Katika taarifa iliyotumwa na ofisi ya Waziri Mkuu ilieleza kuwa, Majaliwa alimueleza Rais huyo wa Caf, mikakati ambayo Serikali inatumia ili kuinua kiwango cha soka nchini.

“Sisi tumeanza kuboresha michezo nchini chini ya mpango unaohusisha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Ofisi ys Rais TAMISEMI na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mpango huu unalenga kuibua vipaji vya vijana kupitia mashindano ya UMITASHUMTA, UMISETA, Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati,” alisema Majaliwa

Aidha katika hatua nyingine Majaliwa alimueleza Rais huyo wa Caf kuwa, nchi nyingi zimeshindwa kufanya vizuri kwenye michezo kwa kuwa serikali zao hazitengi bajati kwenye nyanja hiyo.

“Nimemweleza kuwa hapa kwetu kupitia Bunge letu tukufu, tumekuwa tukitenga bajeti hiyo japokuwa tunajua kuwa haitoshelezi mahitaji yote.

“Kuhusu uendelezaji wa michezo nchini, Rais wa CAF ametusihi tuwe na mpango madhubuti wa kupata maeneo ya kufanyia mazoezi, tuwe na viwanja bora vyenye vipimo vya kisasa, jambo ambalo nimemweleza linatekelezwa na shirikisho la soka nchini.

“Pili, ametutaka tuandae vijana kuanzia umri mdogo, tuwe na taasisi za Serikali na za sekta binafsi zinazofundisha soka, waamuzi, makocha ili tuwaibue akina Samatta wengi zaidi kwani na sisi tunaamini kuwa wapo,” alinena Majaliwa.

Kwa upande wa Dk. Motsepe alinena kuwa katika uongozi wake kama Rais wa Caf, amelenga mambo matatu ambayo ni haja ya sekta binafsi kuwekeza katika mchezo wa soka na kuongeza Udhamini, ujenzi wa vituo vya michezo na vituo vya kuendeleza vijana nan kusema kuwa “Tunataka na wao wafikie viwango vya kimataifa,”

Katika hatua nyingine Motsepe alisema kuwa timu ya Taifa ya Tanzania, ina uwezo kuwa timu bingwa barani Afrika kutokana na umahiri walionao hivi sasa na ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuunga mkono michezo nchini ambapo wiki ijayo atapokea kombe la CECAFA -2021 la vijana wenye umri chini ya miaka 23.

error: Content is protected !!