October 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa ataka Suma JKT kuongeza kasi ujenzi ofisi za NEC

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, wakati alipokagua Jengo la Ofisi ya Tume ya Uchaguzi (NEC), lililopo Njedengwa, jijini Dodoma

Spread the love

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) linalojengwa na Kampuni ya Ujenzi ya Suma JKT katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea)

Tarehe 18 Novemba, 2019, Waziri Mkuu alitembelea mradi huo na kuonesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa mkandarasi aliyekuwa akijenga jengo hilo ambaye ni Wakala Majengo Tanzania (TBA) na kuagiza kuvunjwa kwa mkataba.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumatano, tarehe 13 Mei, 2020 wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la NEC.

Amesema amefurahishwa na hatua iliyofikiwa na anaamini litakamilika kwa wakati.

“…ninahakika mkiongeza nguvu katika baadhi ya maeneo tutafika na haya ndio Serikali inataka kuona taasisi zake zikifanya. Kwenye jengo hili ndipo Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuchukua fomu,” amesema

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya Ujenzi ya Suma JKT kwa namna walivyoratibu vizuri ujenzi wa jengo hilo. “Miradi mingi waliyokabidhiwa Suma JKT imekuwa ikijengwa kwa weledi mkubwa.”

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua Jengo la Ofisi ya Tume ya Uchaguzi (NEC), lililopo Njedengwa, jijini Dodoma

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema Kampuni ya Ujenzi ya Suma JKT ilikabidhiwa mradi wa ukamilishaji wa jengo hilo tarehe 24 Desemba 2019 na unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Mei  2020.

Amesema mradi huo unaosimamiwa na Chuo Kikuu Ardhi (ARU) kama mshauri wa mradi hadi leo Jumatano ujenzi wa jengo kuu la ofisi umefikia asilimia 85, jengo la kutangazia matokeo ujenzi wake umefikia asilimia 68, kazi za nje zimefikia asilimia 85 huku jengo la ghala limefikia asilimia 92.

Naye, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dk. Wilson Mahera amesema mkataba wa mradi huo ulipaswa ukamilike tarehe 30 Aprili  2020 lakini baada ya kutembelea eneo la mradi wamekubaliana kuwa kazi hiyo iwe imekamilika ifikapo tarehe 30 Mei 2020 na tarehe 1 Juni  2020 watumishi wahamie na kuanza kazi.

Amesema mradi huo unagharimu zaidi ya Sh. 12 bilioni na tayari zaidi ya sh bilioni sita zimeshatolewa na kwamba kazi zinazoendelea kwa upande wa jengo kuu la ofisi ni pamoja na kupachika milango na madirisha, kupaka rangi na kuweka vigae kwenye sakafu.

error: Content is protected !!