March 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa apiga marufuku dawa mbadala

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Spread the love

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itadhibiti matumizi mabaya ya baadhi ya dawa za hospitali na kemikali zinazowekwa katika vyakula, ambazo hutumiwa kama mbadala wa dawa za kulevya. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Akizungumza leo tarehe 17 Septemba  2018 jijini Dar es salaam katika Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Vyombo vinavyopambana na Dawa za Kulevya  kutoka nchi za Afrika, Majaliwa amesema serikali imebaini kwamba kuna wimbi la matumizi mabaya ya dawa na kemikali hizo,  hivyo ina mkakati wa kumaliza matumizi hayo.

Pia, Waziri Majaliwa amesema serikali itaweka mkazo katika kudhibiti vitendo vya baadhi ya wananchi kulima mazao yanayotumika kama dawa za kulevya ikiwemo bangi na mirungi, kinyume na sheria mbapo wamekuwa wakilima kwa kuchanganya na mazao mengine.

“Sasa tumeona upunguaji wa matumizi ya dawa za kulevya zaidi ya asilimia 90. Lakini tumebaini bado kuna matumizi aina ya dawa hata zile zinazotumika hospitalini zinazopelekea watu kupata kilevi. Nayo pia ni mikakati tulioanza nayo, lakini pia kemikali zinazotengeneza baadhi ya dawa kwenye vyakula zinatumika visivyo nayo tumeanza kupambana nayo, malengo yetu tumalize kabisa matumizi ya dawa za kulevya, “ amesema.

Kuhusu mkutano wa Wakuu wa Vyombo vinavyopambana na Dawa za Kulevya  kutoka nchi za Afrika, Waziri Majaliwa amesema Tanzania itautumia mkutano huo katika kupata uzoefu wa kukabiliana na kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya.

“Kikao hiki kitatupa uzoefu zaidi, pia kitatoka na maadhimio pamoja na kuweka mikakati ya kubadilishana mawazo na nchi zetu za Afrika ili tufikie hatua ambayo sasa matumizi ya dawa za keluvya yanapungua,” amesema.

error: Content is protected !!